OFISI YA RAIS
TAWALA ZA MIKOA NA IDARA MAALUM ZA SMZ

OFISI YA MKUU WA MKOA MJINI MAGHARIBI

Home>>Habari>>Matokeo ya Mtihani wa Mock yatoka
HabariHabari Mpya

Matokeo ya Mtihani wa Mock yatoka

Kamati ya Mtihani Timilifu (Mock) ya Mkoa Mjini Magharibi imetoa matokeo ya mtihani huo ya kidatu cha nne mwaka 2023.

Akitangaza matokeo hayo mbele ya waandishi wa habari hapo Skuli ya Sekondari Lumumba, Afisa elimu Mkoa Mjini Magharibi Mohammed Abdalla Mohammed amesema kuwa ufaulu kwa mwaka huu umeongezeka kutoka asilimia 70.2 mwaka 2022 hadi kufikia asilimia 81.6 kwa mwaka 2023.

Mohammed amesema jumla ya wanafunzi 12,356 walifanya mtihani huo ambapo  matokeo kwa ujumla yanaonesha asilimia 81.6 ya watahiwa wamefaulu huku asilimia 18.4 wameshindwa kufaulu mtihani huo.

Amefahamisha kuwa  kati ya wanafunzi waliyofaulu asilimia 9.3 walipata daraja la kwanza, asilimia 9.19 walipata daraja la pili, asilimia 14.54 wamepata daraja la tatu na asilimila 48.61 walipata daraja la nne.

Aidha ameeleza kuwa  kati ya wanafunzi  12,624 waliyoandikishwa kufanya mtihani huo wa utimilifu, wanafunzi  12356 ndio  waliofanya mtihani  ambapo wanawake  walikuwa 7175 na wanaume 5181  

Amesema wanafunzi 268 hawajajikokeza kufanya mtihani huo kwa sababu mbali mbali wakiwemo wanawake 137 na wanaume 131.

Afisa Elimu amesema licha ya ufaulu wa mwaka huu kuongezeka bado kuna haja kwa walimu kuweka mikakati mbali mbali itakayowasaidia wanafunzi kufanya vizuri zaidi katika mtihani wao wa taifa wa kidatu cha nne unaotarajiwa kufanyika mwezi novemba.

‘’ Niwaombe walimu muyatumie matokeo haya kama kipimo cha kuwasaidia wanafunzi waliyoanguka ili nao waweze kufanya vizuri katika mtihani wa taifa’’, alisisitiza Mohammed.

Sambamba na hayo Mohammed ameeleza kuwa katika kuhakikisha lengo hilo linafikiwa Mkoa umeandaa mtihani mwengine utakaofanywa na wanafunzi wote wa kidatu cha nne unaujulikana kama Jiepushe na Zero ili kuweza kuwapima wanafunzi kwa mara nyengine kabla kufanya mtihani wa kuingia kidatu cha tano.

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Mitihani ya Moko ya Mkoa Mjini Magharibi Mussa Hassan Mussa amesema upo uwezekano mkubwa wa kupunguza idadi ya wanafunzi waliyofanya vibaya ikiwa wazazi na walimu watashirikiana katika kuwasimamaia wanafunzi.

Vilevile amewapongeza baadhi ya Walimu Wakuu wa Skuli mbali mbali za Mkoa huo ikiwemo Skuli ya Sekondari ya Mtopepo kwa kupunguza idadi ya wanafunzi wasiofanya mtihani huo ikilinganishwa na miaka ya nyuma.