Imeelezwa kuwa ushiriki mkubwa wa wananchi wa Mkoa Mjini Magharibi katika usafi wa mazingira kumeonesha ni kwa kiasi gani wanavyounga mkono Mapinduzi ya Zanzibar ya Januari 1964
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Idrissa Kitwana Mustafa katika shamra shamra za Maadhimisho ya miaka 59 ya Mapinduzi ya Zanzibar zilizoanza kwa usafi wa mazingira kwenye Wilaya, Manispaa na Halmashauri zote Unguja na Pemba.
Akizungumza na wananchi kwa nyakati tofauti katika Wilaya tatu za Mkoa wake wakati aliposhiriki katika usafi wa mazingira, Mkuu wa Mkoa amesema zoezi hilo limefanikiwa kutokana na namna viongozi wa majimbo, wadi, masheha pamoja na wananchi walivyoshiriki.
Aidha Idrissa amewaomba wananchi kuhudhuria kwa wingi katika uwekaji wa mawe ya msingi na uzinduzi wa miradi katika maadhimisho hayo. Amesema baadhi ya miradi hiyo katika Mkoa Mjini Magharibi itazinduliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi.
Nao wananchi walioshiriki zoezi hilo wamesema suala la usafi wa ni muhimu, hivyo wameamua kushirikiana na viongozi wao wa Mkoa, Wilaya, jimbo na shehia ili kuuweka mji katika hali nzuri hasa kipindi hiki cha Maadhisho ya miaka 59 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Wakati huo huo zoezi la usafi wa mazingira limefanyika katika majengo ya taasisi za Serikali na barabara kuu mbali mbali lilowashirikisha wafanyakazi na askari wa vikosi vya SMZ.