OFISI YA RAIS
TAWALA ZA MIKOA NA IDARA MAALUM ZA SMZ

OFISI YA MKUU WA MKOA MJINI MAGHARIBI

Home>>Habari>>Hali ya Ulinzi yaimarisha. RC Kitwana
HabariHabari Mpya

Hali ya Ulinzi yaimarisha. RC Kitwana

Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Uhamasishaji ya Maadhimisho ya Sherehe za Miaka 60 ya Mapinduzi ya Zanzibar Mhe.Idrissa Kitwana Mustafa amesema hali ya ulinzi imezidi kuimarishwa ndani ya Mkoa huo katika kipindi hiki kuelekea kilele cha Maadhimisho hayo.

Amesema hayo wakati akitoa taarifa yake mbele ya vyombo vya habari  kuhusu kilele cha Maadhimisho ya Miaka 60 ya Mapinduzi ya Zanzibar yatakayofanyika tarehe 12 Januari 2024 katika Uwanja wa New Amani Complex.

Amewahakikishia wananchi na wageni watakaohudhuria sherehe hizo kuwa hali ya Mkoa huo itaendelea kuwa salama wakati vyombo vya ulinzi vikiendelea kufanya doria zake katika maeneo mbalimbali ndani na nje ya mji.

Wakati huo huo Mkuu huyo wa Mkoa amewahimiza wananchi wa Mkoa huo na Mikoa mingine jirani kuhudhuria kwa wingi katika Maadhimisho hayo ambayo amesema safari hii yatakuwa ni ya aina yake kutokana na matukio kadha wa kadha yaliyoandaliwa.

Mhe.Idrissa amesema sherehe za kilele zitafanyika saa 8:00 mchana na milango  itakuwa wazi kuanzia saa 4:00 asubuhi  ili kwa wale watakaofika mapema waweze kuingia uwanjani.

Amesema kutokana na sababu mbali mbali Serikali imeamua kufanya shughuli hiyo kuanzia wakati wa mchana ili kuwapa nafasi wananchi waliowengi waweze kuhudhuria katika Maadhimisho hayo.

Sambamba na hayo Mkuu wa Mkoa amewaomba wananchi kuhudhuria katika Tamasha la burudani na Fashfashi litakalofanyika katika viwanja vya Maisara siku ya Alkhamis tarehe 11Januari, 2024 kuanzia saa 1:00 usiku ambapo viongozi mbali mbali wanatarajiwa kuhudhuria.

Zanzibar inasherehekea Miaka 60 ya Mapinduzi tangu yalipofanyika tarehe 12 Januari, 1964.