OFISI YA RAIS
TAWALA ZA MIKOA NA IDARA MAALUM ZA SMZ

OFISI YA MKUU WA MKOA MJINI MAGHARIBI

Home>>Habari>>Maafisa Utumishi simamieni nidhamu kazini – RAS Mohamed
HabariHabari Mpya

Maafisa Utumishi simamieni nidhamu kazini – RAS Mohamed

Maafisa Utumishi Mkoa wa Mjini Magharibi wametakiwa kusimamia vyema majukumu yao ili kuleta ufanisi katika utekelezaji wa kazi na kudumisha nidhamu kwa wafanyakazi wao.

Akizungumza na Maafisa hao katika kikao kazi kwenye ukumbi wa Afisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Katibu Tawala Mkoa huo Ndugu Mohamed Ali Abdalla amesema kuwa ni wajibu wa Maafisa hao kuwasimamia wafanyakazi wao kwa kuhakikisha uwepo wa utendaji kazi wenye  nidhamu na uwajibikaji   ili kutekeleza nyema kazi zao kwa kiwango kinachostahiki.

Amesema kuwa afisi yake itahakikisha kuwa kila mtumishi anawajibika ipasavyo kwenye jukumu lake alilopangiwa na kuwataka Maafisa Utumishi kusimamia wajibu wao wa kazi ili dhamira ya serikasli iweze kufikiwa.

Aidha amewataka Maafisa Utumishi hao  kufanya kazi kwa mashirikiano na kupeana taarifa miongoni mwao sambamba na kubadilisha uzowefu huku akiahidi kuwa Afisi yake  inawapatia  kila aina ya mahitaji wanayoyataka kwa dhamira ya  kuwasimamia wafanyakazi wao wanawaongoza katika maeneo yao ya kazi

Akizungumzia kuhusu suala la umuhimu wa mafunzo kwa Maafisa Utumishi Ndugu Mohamed amewaahidi Maafisa hao kuwapatia taaluma stahiki zitakazoendana na utendani wa kazi zao kwa kuzingatia mabadiliko ya Teknolojia nchini.

Kwa upande wao Maafisa hao wameomba kupatiwa mafunzo ya Ujengaji Uwezo sanjari na ziara za mafunzo ndani na nje ya nchi ili kuongeza ujuzi, elimu na taaluma ya kazi zao

Aidha wameushukuru uongozi wa Afisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi kwa jitihada zake za kuzipatia ufumbuzi changamoto mbalimbali zinazowakabili   katika maeneo yao ya kazi. Kikao kazi hicho kiliwahusisha Maafisa Utumishi kutoka Baraza la Manispaa  Mjini, Baraza la Manispaa Magharibi “A”, Baraza la Manispaa Magharibi “B” Pamoja na Maafisa Utumishi wa Wilaya zote zilizomo ndani  ya Mkoa wa Mjini Magharibi