OFISI YA RAIS
TAWALA ZA MIKOA NA IDARA MAALUM ZA SMZ

OFISI YA MKUU WA MKOA MJINI MAGHARIBI

Home>>Habari>>RC apongeza mshirikiano yaliyooneshwa Mwenge wa Uhuru 2023
HabariHabari Mpya

RC apongeza mshirikiano yaliyooneshwa Mwenge wa Uhuru 2023

Mwenyekiti wa Kamati ya Usalama ya Mkoa Mjini Magharibi ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa huo Mhe. Idrissa Kitwana Mustafa amepongeza mashirikiano makubwa yaliyooneshwa na viongozi na watendaji katika mbio za Mwenge wa Uhuru ndani ya Mkoa huo  mwaka 2023.

Pongezi hizo amezitoa mara baada ya Kamati ya Usalama kupokea taarifa  ya tathmini kuhusu mbio hizo kutoka kwa maofisa wa sekta mbali mbali pamoja na waratibu wa Mwenge wa Uhuru wa Mkoa na Wilaya zake.

Amesema kutokana na mashirikiano hayo Mkoa wake umeweza kufanya vizuri katika mbio hizo ndani ya Wilaya zake zote tatu za Mkoa huo zilizoanza tarehe 29 hadi 31 Mei 2023.

Aidha ameeleza kuwa ubunifu uliyooneshwa na watendaji wa Mkoa na Wilaya umekuwa chachu ya kufanikisha mbio hizo kwa mwaka huu.

Mkuu huyo wa Mkoa amewataka viongozi ,watendaji  pamoja na waratibu wa Mwenge kuendeleza mashirikiano hayo ili kuweza kufanya vizuri zaidi katika mbio za Mwenge wa Uhuru hapo mwakani.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Magharibi ‘A’ Mhe. Susan Peter Kunambi amesema kwamba muongozo na maelekezo mazuri waliyoyapata kutoka kwa uongozi wa Mkoa ndio yaliyopelekea mafanikio katika mbio hizo.

Aidha wameishukuru Kamati ya Usalama ya Mkoa kwa ushauri wao katika kupitisha miradi iliyotembelewa wakati wa mbio hizo.

Kwa upande wao Maofisa walioshiriki kwenye mbio hizo wameeleza kuwa kuwa safari hii waliweza kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi wa hali ya juu kutokana na mashirikiano makubwa waliyoyapata kwa viongozi wa Mkoa na Wilaya tangu wakati wa maandalizi hadi mwisho wa mbio hizo. 

Kikao hicho kilipokea taarifa kutoka kwa wakimbiza Mwenge wa Uhuru Kimkoa, wasimamizi wa usafiri, Maofisa wa Afya na waratibu wa Mwenge wa Mkoa na Wilaya.