Waziri Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa amewataka watanzania kuisoma lugha ya Kiswahili ili kunufaika na fursa mbali mbali zitokanazo na lugha hiyo.
Amesema licha ya kuwa lugha ya Kiswahili chimbuko lake ni Tanzania hata hiyo bado Watanzania hawajanufaika ipasavyo na fursa zilizopo ulimwenguni ukilinganisha na mataifa mengine ambayo hayazungumzi kiswahili kama ilivyo hapa nchini.
Wito huo ameutoa alipokuwa akifungua Maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani hapo ukumbi wa Chuo cha Polisi Ziwani.
Akizungumzia juu ya kuikuza lugha hiyo, Mheshimiwa Majaliwa ameziagiza Wizara zenye dhamana ya kusimamia lugha ya Kiswahili kuweka mikakati iliyo wazi katika kukikuza kiswahili sambamba na kutoa motisha kwa wanafunzi watakaofaulu vizuri kama ilivyo kwa masomo ya sayansi.
Sambamba na hilo amelitaka Baraza la Kiswahili Tanzania (BAKITA) na Baraza la Kiswahili Zanzibar (BAKIZA), kuhakikisha lugha ya kiswahili inakuwa na kuwanufaisha Watanzania kwa kupata nafasi za kwenda kufundisha katika vyuo mbali mbali ulimwenguni.
Aidha amepongeza mijadala na makongamano yaliyofanyika takika kuadhimisha Siku ya Kiswahili Duniani ambayo amesema yataamsha ari kwa wataalamu na wazungumzaji wa Kiswahili kuiendeleza lugha hiyo.
Aidha Waziri Mkuu amewataka watanzania waone faghari kuzungumza kiswahili kutokana heshima iliyopewa lugha hiyo na Shirika la Umoja wa Mataifa la Sayansi na Utamaduni (UNESCO), kwa kuadhimishwa kimataifa ifikapo tarehe 7 Julai ya kila mwaka.
Katika hafla hiyo wanafunzi waliyoshinda nafasi ya kwanza katika uandishi wa Insha kutoka Tanzania Bara na kutoka Zanzibar walizawadiwa zawadi mbali mbali na fedha taslim shilingi laki tano kila mmoja.