OFISI YA RAIS
TAWALA ZA MIKOA NA IDARA MAALUM ZA SMZ

OFISI YA MKUU WA MKOA MJINI MAGHARIBI

Home>>Habari>>RC Kitwana aishukuru Benki ya Dunia
HabariHabari Mpya

RC Kitwana aishukuru Benki ya Dunia

Uongozi wa Mkoa Mjini Magharibi umeishukuru Benki ya Dunia kwa uamuzi wake wa kukaa pamoja na viongozi na watendaji wa Serikali  ngazi ya Mikoa na Wilaya kwa ajili ya kuwasilisha mwongozo wa miradi mbali mbali itakayofadhiliwa na Benki hiyo kwa mwaka 2024 hadi 2029.

Shukurani hizo zimetolewa na Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Idrissa  Kitwana Mustafa wakati ujumbe kutoka Benki hiyo ukiongozwa na Mwakilishi wa Benki ya Dunia Nchini Tanzania Bi. Makiko Watanabe ulipofika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa hapo Vuga kuelezea juu ya mwongozo huo.

Akizungumza katika Kikao hicho ambacho kilishirikisha pia viongozi na watendaji wa Mikoa mengine, Mkuu wa Mkoa amesema hatua hiyo itasaidia kuona miradi inayokwenda kutekelewa inafahamika na Mikoa tangu hatua za awali.

Ameuhakikishia ujumbe huo kuwa Mikoa itashirikiana na sekta zote husika ili kuona mipango iliyolengwa kutekelezwa katika kipindi hicho inafanikiwa.

Vilevile ameipongeza Benki hiyo kwa kuendelea kuziunga mkono Serikali zote mbili katika utekelezaji wa miradi mbali mbali ikiwemo miradi mikubwa ya kimkakati.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja Ayoub Mohammed Mahmoud  amesema Serikali za Mitaa zimekuwa zikifanya kazi karibu na wananchi hivyo ameiomba Benki hiyo kuangalia uwezekano wa kuzijengea uwezo  kwa upande wa utaalamu na vitendea kazi.

Mwakilishi wa Benki ya Dunia Nchini Tanzania Bi. Makiko Watanabe  amesema Benki hiyo imepanga kutumia kiasi cha Dola za Marekeni Bilioni 2 kwa Tanzania kwa mwaka 2024-2029 katika maeneo matatu makuu ikiwemo kuimarisha huduma muhimu za jamii , miundombimu na programu za kuiwezesha jamii.

Amesema ili kufikia lengo hilo Benki yake imeona kuna haja ya kukutana na wadau mbali mbali ili kupitia mwongozo wa miradi itakayotekelezwa na namna fedha hizo  zitakavyotumika katika sekta mbali mbali .