OFISI YA RAIS
TAWALA ZA MIKOA NA IDARA MAALUM ZA SMZ

OFISI YA MKUU WA MKOA MJINI MAGHARIBI

Home>>Habari>>Wastaafu watarajiwa angalieni fursa za miradi – RC Kitwana
HabariHabari Mpya

Wastaafu watarajiwa angalieni fursa za miradi – RC Kitwana

Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Mhe.Idrissa Kitwana Mustafa amewataka wastaafu watarajiwa kuangalia fursa za miradi katika sekta ya uchumi wa buluu, kilimo na ujasiriamali ili kujiwezesha kiuchumi kwa dhamira ya kuendesha maisha yao.

Amesema lengo la Serikali ya awamu ya nane kupitia uchumi wa buluu ni kuwakwamua wananchi kiuchumi.

Mkuu wa Mkoa amesema hayo huko katika ukumbi wa sheikh Idrissa Abdul Wakil Kikwajuni wakati akifungua mafunzo ya siku mbili ya maandalizi ya kustaafu kwa wastaafu watarajiwa wa mfuko wa hifadhi ya jamii kwa watumishi wa umma  (PSSSF).

Amesema ni vyema kwa watumishi wa umma kujiandaa katika kukusanya kipato kwa lengo la kuwasaidia wanapostaafu na kwa maslahi mazuri ya maisha yao ya baadae.

Mhe .Idrissa amewasisitiza wastaafu hao wanaotarajiwa kumaliza mda wao wa utumishi kuyatumia mafunzo hayo waliyopatiwa katika kuleta matokeo chanya.

Aidha amesema anaimani kuwa mafunzo hayo yatawajengea wastaafu hao watarajiwa elimu endelevu katika kukuza kipato chao.

Mapema Kaimu Mkurugenzi Mkuu Mfuko wa hifadhi ya jamii kwa watumishi wa umma ambae pia ni mshika fedha Ndg. Bitris Lupi amesema kuwa mfuko huo una dhamira ya kuwahudumia wananchi wanaotumia pencheni zao baada ya kustaafu .

Kadhalika amesema wamekuwa wakitoa elimu kwa wastaafu wanaomaliza mda wao wa utumishi ili kupata fedha zao kwa urahisi na kuepukana na changamoto za upotevu wa fedha kupitia miamala yao.

Akitoa shukrani kwa niaba ya wanachama wenzake Ndugu Makame Khatibu ameipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar , Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na mfuko wa PSSSF kwa kuwapatia mafunzo na kuahidi kuyafanyia kazi mafunzo hayo yenye dhamira ya kuwawezesha kimaendeleo.

Mfuko wa PSSSF umeanzishwa mwaka  2018 ambapo kiasi cha wafanyakazi wapatao elfu 21 katika Mikoa yote hapa nchini wanatarajiwa kustaafu katika kipindi cha mwaka 2023 hadi 2024.