OFISI YA RAIS
TAWALA ZA MIKOA NA IDARA MAALUM ZA SMZ

OFISI YA MKUU WA MKOA MJINI MAGHARIBI

Home>>Habari>>Ujenzi soko la Mwanakwerekwe waendelea kwa kasi
HabariHabari Mpya

Ujenzi soko la Mwanakwerekwe waendelea kwa kasi

Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Mhe. Idrissa Kitwana Mustafa amewataka wafanyabiashra wa Soko la muda la Mwanakwerekwe kuendelea kuwa wastahamilivu wakati ujenzi wa Soko jipya la Mwanakwerekwe ukiendelea.

Mkuu wa Mkoa ametoa ombi hilo wakati alipofanya ziara yake kukagua hali ya biashara pamoja na kuzungumza na wafanyabiashara katika Soko hilo la muda la Mwenakwerekwe, Wilaya ya Magharibi B.

Amewaeleza wafanyabiashara hao kuwa changamoto iliyosababisha kusita kwa ujenzi wa Soko jipya la Mwanakwerekwe tayari Serikali imeshaipatia ufumbuzi na kwa sasa kazi ya ujenzi wa Soko hilo inaendelea kwa kasi na inatarajiwa kukamilika ndani ya muda uliyopangwa.

Mkuu wa Mkoa amewahakikishia wafanyabishara wote waliokuwepo katika Soko la Mwanakwerekwe kabla ya kuvunjwa kwamba watarudi katika Soko jipya pale ujenzi wake utakapokamilika na nafasi zitakazobaki watapatiwa wafanyabiashara wengine waweze kuendelea na biashara zao.

Aidha Mhe. Idrissa amewataka  wafanyabiashara hao kutopandisha bei za vyakula wakati mwezi mtukufu wa Ramadhani ukikaribia ili kuwawezesha wananchi kumudu kununua bidhaa hizo.

Amesema Serikali isingependa kuona baadhi ya wafanyabishara wanautumia mwezi wa Ramadhani kwa ajili ya kujipatia faida zaidi badala ya kuwafanyia tahafifu wananchi katika kupata bidhaa muhimu za chakula.

Nao wafanyabiashara hao wamemuomba Mkuu wa Mkoa kulipatia ufumbuzi tatizo la kutuwama  kwa  maji wakati wa mvua hali inayopelekea usumbufu na kukimbiza wateja katika soko hilo la muda la Mwanakwerekwe. 

Ujenzi wa Soko jipya la Mwanakwerekwe linalojengwa  na Jeshi la Kujenga Uchumi (JKU), utagharimu kiasi cha shilingi bilioni 27 na unatarajiwa kukamilika mwaka 2024.