OFISI YA RAIS
TAWALA ZA MIKOA NA IDARA MAALUM ZA SMZ

OFISI YA MKUU WA MKOA MJINI MAGHARIBI

Home>>Habari>>Mwenge wa Uhuru wakabidhiwa Mkoa wa Kusini.
HabariHabari Mpya

Mwenge wa Uhuru wakabidhiwa Mkoa wa Kusini.

Mkuu wa Mjini Magharibi Idrissa Kitwana Mustafa amekabidhi Mwenge wa Uhuru kwa Mkuu wa Mkoa Kusini Unguja Rashid Hadid Rashid   baada ya kumaliza mbio zake katika Wilaya tatu za Mkoa Mjini Magharibi.

Akisoma Taarifa ya Makabidhiano ya Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2023, Mkuu wa Mkoa  amewashukuru Viongozi Wakuu wa Kitaifa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi  kwa maono yao makubwa na dhamira njema za kuwaletea maendeleo wananchi wa Zanzibar na Tanzania  kwa ujumla.

Amesema kwamba miradi mikubwa ya kimkakati inaendelea kutekelezwa katika sekta mbali mbali ndani ya Mkoa wa Mjini Magharibi ikiwemo ya  afya,elimu, maji, na miundombinu mengineyo ambayo inakwenda kuimarisha huduma muhimu za kijamii.

Amefahamisha kwamba jumla ya miradi hiyo 15 na shughuli 4  yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 118 imepitiwa na Mwenge wa Uhuru 2023 kukagua ujenzi wake na  ile iliyokwisha anza kutoa huduma kwa wananchi.

Akizungumzia ujumbe wa Mwenge wa Uhuru juu ya uhifadhi wa mazingira  Idrissa amesema  miti 49,797 ya matunda, bustani na misitu imepandwa  maeneo ya fukwe za bahari, barabara kuu na vyanzo vya maji kabla ya mbio za Mwenge kwenye Mkoa huo.

Aidha amesema misumeno 14 ya moto inayotumika bila ruhusa imekamatwa, wafanyabiashara 27 wanaouza mifuko ya plastiki na wavuvi 204 wanaojishughulisha na uvuvi haramu nao wamekamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.

Kuhusu  suala la malaria, madawa ya kulevya na rushwa  Mkuu wa Mkoa amesema kwamba licha mafanikio yaliyopatikana, Mkoa kwa kushirikiana na Mamlaka husika wanaendelea na mapambano juu ya masuala hayo sambamba na kuelimisha jamii.

Aidha Mkuu wa Mkoa  alieleza  kwamba hali ya usalama kwa mwaka 2022/2023 ndani ya Mkoa wake niyakuridhisha sana ambapo wananchi wanaendelea na shughuli zao mbali mbali za  kujiletea maendeleo na zile za kujipatia kipato katika hali ya amani.

Makabidhiano ya Mwenge wa Uhuru yalifanyika huko Tunguu Mkoa wa Kusini Unguja.