Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Idrissa Kitwana Mustafa amesema uwepo wa Kanuni ya Makaazi ya Watalii kutasaidia kuthibiti matumizi ya nyumba zinazolaza wageni kwenye Shehia.
Amesema hayo wakati akifungua mkutano wa kupokea maoni ya Masheha wa Mkoa Mjini Magharibi kuhusu Kanuni ya Makaazi ya Watalii uliyofanyika ukumbi wa Sheikh Idrissa Abdul Wakil, Kikwajuni.
Amesema kwamba Masheha kama viongozi wa Serikali ngazi ya shehia wanafahamu hali halisi ilivyo katika Shehia zao hivyo uamuzi wa Kamisheni ya Utalii kupokea maoni yao kutasaidia kuiboresha kanuni hiyo.
Mkuu wa Mkoa ameihakikishia Kamisheni ya Utalii kuwa Mkoa utatoa kila aina na mashirikiano ili kuona kanuni hiyo inasimamiwa ipasavyo ndani ya Mkoa wake.
Wakati huo huo Mkuu wa Mkoa aliwataka Masheha kutoa maoni yao yatakayosaidia kuiboresha Kanuni hiyo.
Amesema kwamba zipo nyumba katika Shehia zao zinazotumika kulaza wageni bila kufuata sheria na kupelekea kuikosesha mapato Serikali, hivyo aliwataka Masheha kuzitambua nyumba hizo pamoja na wageni wanaoingia.
Akiwasilisha Kununi ya Makaazi ya Watalii mwanasheria kutoka Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale Mustafa Omar Abdalla amesema Serikali imeamua kuweka kanuni hiyo ili nyumba hizo zifanye biashara kwa mujibu wa taratibu na kuiwezesha Serikali kuingiza kipato.
Vilevile amesema kanuni hiyo imewekwa kwa makusudi ili kuona nyumba zinazolaza watalii zinakidhi sifa na kuhakikisha usalama wa wageni hao.