OFISI YA RAIS
TAWALA ZA MIKOA NA IDARA MAALUM ZA SMZ

OFISI YA MKUU WA MKOA MJINI MAGHARIBI

Home>>Habari>>Ujenzi wa Minara na Vituo vya Tehama Wakamilika Kwenye Mikoa Mitano ya Zanzibar
HabariHabari Mpya

Ujenzi wa Minara na Vituo vya Tehama Wakamilika Kwenye Mikoa Mitano ya Zanzibar

Jumla ya vituo 11 vya tehama na minara ya mawasilianao 42 ambayo imegharimu shilingi bilioni 6.9  imejengwa katika Wilaya zote za Unguja na Pemba  kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote USCAF.

Akizinduzia mnara huko Kisakasaka  na kituo cha tehama huko Bweleo kwa niaba ya mikoa mitano ya Zanzibar, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema kukamilika kwa ujenzi wa minara  hiyo kutaondoa malalamiko ya wananchi  kuhusu tatizo la  mawasiliano ya simu na mtandao.

Amesema wakati wa ziara zake  alizozifanya katika mikoa  alipokea malalamiko kutoka kwa wananchi kwenye baadhi ya maeneo na kuwaahidi kuwa Serikali itaipatia ufumbuzi  changamoto hiyo.

Dk. Hussein ameeleza kufurahishwa kwake kwa kufanikisha miradi hiyo na ameziagiza Wizara husika kukaa pamoja na kufanya tathmini ya maeneo ambayo bado yanakabiliwa na tatito la mawasiliano ili Serikali iweze nayo kuyapatia ufumbuzi.

Aidha amesema kukamilika kwa ujenzi wa vituo vya tehama katika kila Wilaya kutaleta manufaa makubwa kwa wananchi pamoja na kuchochea matumizi ya tehama ambayo ni muhimu kwa huduma za kijamii.

Wakati huo huo Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi amefungua Mkutano wa Sita wa Mwaka wa Tehama Tanzania katika Hoteli ya Golden Tulip Kiembe Samaki na  kuwataka washiriki wa mkutano huo kubainisha fursa zilizopo katika teknolojia ya habari na mawasiliano na changamoto zake ili ziweze kupatiwa ufumbuzi.

Amesema kufuatia janga la Korona dunia imetanabahi juu ya umuhimu wa matumizi ya tehama, hivyo Serikali  ya Mapinduzi ya Zanzibar nayo imeamua kutumia teknolijia hiyo kukuza uchumi wake.

Akiwakaribisha wageni na washiriki  kwenye mkutano huo, Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Idrissa Kiwana Mustafa amesema wakati umefika kwa tehama kutumika katika mfumo mzima wa maisha.

Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja Ayoub Mohammed Mahmoud na Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja Rashid Hadid Rashid nao walihudhuria kwenye matukio hayo.