Wananchi wa Mkoa Mjini Magharibi wameishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Japan kwa ujenzi wa Diko na Soko la kisasa la Samaki Malindi.
Wamesema ujenzi wa Soko hilo unakwenda kuwapatia suluhisho la kudumu kwa wavuvi, wachuuzi wa samaki pamoja na wananchi wa Mkoa huo.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Idrissa Kitwana Mustafa wakati akitoa salamu za wananchi wa Mkoa huo katika uzinduzi wa Diko na Soko la Samaki Malindi.
Amesema Mkoa utahakikisha wachuuzi wa Samaki waliokuwepo kabla ya ujenzi wa Soko hilo wanapewa kipaumbele kurudi kwenye Soko jipya na nafasi zitakazosalia watapatiwa wananchi wengine.
Akizungumzia kuhusu usimamizi wa Soko, ldrissa amesema Mkoa utakaa pamoja na Wizara ya Uvuvi na Uchumi wa Buluu ili kupata mwekezaji atakaeshirikiana na Baraza la Manispaa Mjini kuliendesha Soko hilo.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Uvuvi na Uchumi wa Buluu Aboud Suleiman Jumbe amesema zaidi ya watu 6,500 watanufaika na Soko hilo wakiwemo wavuvi, wachuuzi, wafanyabiashara na shughuli nyengine.
Jumla ya Dola za marekani milioni 14.7 zimetumika kwa ujenzi wa Soko hilo ambapo Serikali ya Japan imetoa dola milioni 13.1na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar 1.6 milioni.
Awali Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi alizindua Soko hilo akiwa katika muendelezo wa uwekaji wa mawe ya msingi na uzinduzi wa miradi ya maendeleo katika Maadhimisho ya Miaka 59 ya Mapinduzi ya Zanzibar.