OFISI YA RAIS
TAWALA ZA MIKOA NA IDARA MAALUM ZA SMZ

OFISI YA MKUU WA MKOA MJINI MAGHARIBI

Home>>Habari>>Rais Samia aipongeza SMZ
HabariHabari Mpya

Rais Samia aipongeza SMZ

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imepongezwa kwa usimamizi mzuri wa fedha za UVIKO 19  zilizototumika kwa ujenzi wa miradi ya maendeleo kwa sekta mbali mbali.

Pongezi hizo zimetolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan alipokuwa akiwahutubia viongozi na wananchi wa Mkoa Mjini Magharibi waliohudhuria uzinduzi wa Skuli ya msingi ya Dkt. Samia  iliopo Mwanakwerekwe  Wilaya ya Magharibi B.

Amesema kwamba fedha hizo zimetumika ipasavyo na zimeleta manufaa makubwa kwa kuweza kufanikisha ujenzi wa miradi  ya afya, elimu, barabara pamoja na sekta nyenginezo ambazo zitaimarisha huduma za kijamii.

Ameeleza kuridhishwa kwake na utekelezaji wa miradi hiyo na kuwataka watendaji kukamilisha miradi iliyobaki ili wananchi waweze kunufaika nayo.

Kwa upande mwengine Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ameitaka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kuweka mikakati itakayoweza kuinua kiwango cha elimu hapa Zanzibar ili wanafunzi waweze kufanya vizuri katika mitihani yao ya kitaifa. Amesema bado  Zanzibar haifanyi vyema katika mitihani hiyo jambo ambalo Wizara inatakiwa kuhakikisha inalifanyia kazi ili kuondokana na hali hiyo.

Ameeleza kuvutiwa na miundo mbinu ya maabara, chumba cha kompyuta na maktaba iliyomo katika Skuli hiyo ya msingi na kusema kuwa itaweza kuwajenga mapema wanafunzi katika masomo ya sayansi na matumizi ya tehama na kuiagiza Wizara ya Elimu kuhakikisha mafunzo hayo yanakuwa endelevu.

Aidha Dkt. Samia amewahimiza wazazi na walezi kuwasimamia watoto wao katika matumizi ya simu na kuwataka wazitumie kwa kuingiza programu za elimu  badala ya kutumia kwa mitandao ya kijamii isiyo na faida.

Akitoa salamu za wananchi, Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Idrisa Kiwana Mustafa amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi kwa kuelekeza fedha za UVIKO kutumika katika ujenzi wa miundo mbinu mbali mbali ndani ya Mkoa wake.

Amesema kupitia fedha hizo  zaidi ya shilingi bilioni 28 zimetumika kwenye sekta ya elimu katika Mkoa Mjini Magharibi kwa ujenzi wa Skuli 5 za horofa , madarasa mapya 118, vyoo 329, kukamilisha ujenzi wa madarasa 40 yaliyojengwa kwa nguvu za wananchi na  Skuli 5 zimefanyiwa ukarabati. Amesema hayo ni mafanikio makubwa yaliyopatikana ndani ya Mkoa wake kwa kipindi cha mwaka mmoja.

Naye Waziri wa Elimu na Mafuzo ya Amali Lela Mohammed Mussa amesemaa kiasi cha shilingi bilioni 83 ya fedha za UVIKO zimetumika katika sekta ya elimu Zanzibar kwa ujenzi wa miundo mbinu ya skuli, vikalio na vitendea kazi vyengine. Amesema uwekezaji huo ni mkubwa na kuahidi kuwa Wizara yake watausimamia ili kuona wanafunzi wanakuja na matokeo mazuri ya mitihani yao.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan aliizindua rasmi skuli hiyo yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi takriban 1,300 ambayo imegharimu shilingi bilioni 4.3