Imeelezwa kuwa kuanza kutumika kwa Soko jipya la Samaki la Malindi kumeinua kipato cha wachuuzi na wafanyabiashara wa soko hilo tangu lifunguliwe rasmi mwezi januari mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Malindi, Mkuu wa Soko hilo Ame Khatib Kombo amesema hali ya biashara imekuwa ikiimarika siku hadi siku kwenye Soko hilo.
Aidha, amesema uwepo wa majokofu ya kuhifadhia Samaki katika Soko la Malindi yenye uwezo wa kuhifadhi Samaki hadi tani 100 kumewawezesha wachuuzi na wafanyabiashara kupata nafasi ya kutosha ya kuhifadhia samaki wao na hivyo kuwaepusha kuwauza kwa hasara.
Kadhalika Mkuu huyo wa Soko amefafanua juu ya ulipaji kodi ambapo kila mfanyabiashara hulipa kiasi cha shilingi 1000/= kwa siku kama malipo kwa ajili ya uendeshaji wa Soko.
Kwa upande wake mmoja wa wafanyabiashara Khamis Talib Saleh ameeleza kufurahishwa kwa hatua kubwa iliyochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kujenga Soko hilo la kisasa.
Soko jipya la Samaki Malindi lilifunguliwa rasmi na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi katika shamra shamra za kutimiza miaka 59 ya Mapiduzi ya Zanzibar.