OFISI YA RAIS
TAWALA ZA MIKOA NA IDARA MAALUM ZA SMZ

OFISI YA MKUU WA MKOA MJINI MAGHARIBI

Home>>Habari>>Biashara Soko la Samaki Malindi yaimarika
HabariHabari Mpya

Biashara Soko la Samaki Malindi yaimarika

Imeelezwa kuwa kuanza kutumika kwa Soko jipya la Samaki la Malindi kumeinua kipato cha wachuuzi na wafanyabiashara wa soko hilo tangu lifunguliwe rasmi mwezi januari mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Malindi, Mkuu wa Soko  hilo Ame Khatib Kombo amesema hali ya biashara imekuwa ikiimarika siku hadi siku kwenye Soko hilo.

Aidha, amesema uwepo wa majokofu ya kuhifadhia Samaki katika Soko la Malindi  yenye uwezo wa kuhifadhi Samaki hadi tani 100 kumewawezesha wachuuzi na wafanyabiashara kupata nafasi ya kutosha ya kuhifadhia samaki wao na hivyo kuwaepusha kuwauza kwa hasara.

Kadhalika Mkuu huyo wa Soko amefafanua juu  ya ulipaji kodi ambapo kila mfanyabiashara hulipa kiasi cha shilingi 1000/= kwa siku kama malipo kwa ajili ya uendeshaji wa Soko.

Kwa upande wake mmoja wa wafanyabiashara Khamis Talib Saleh ameeleza kufurahishwa kwa hatua kubwa iliyochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kujenga Soko hilo la kisasa.

Soko jipya la Samaki Malindi  lilifunguliwa rasmi na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi katika shamra shamra za kutimiza miaka 59 ya Mapiduzi ya Zanzibar.