Maafisa Utumishi Mkoa wa Mjini Magharibi wametakiwa kusimamia vyema majukumu yao ili kuleta ufanisi katika utekelezaji wa kazi na kudumisha nidhamu kwa wafanyakazi wao.
Akizungumza na Maafisa hao katika kikao kazi kwenye ukumbi wa Afisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Katibu Tawala Mkoa huo Ndugu Mohamed Ali Abdalla amesema kuwa ni wajibu wa Maafisa hao kuwasimamia wafanyakazi wao kwa kuhakikisha uwepo wa utendaji kazi wenye nidhamu na uwajibikaji ili kutekeleza nyema kazi zao kwa kiwango kinachostahiki.
Amesema kuwa afisi yake itahakikisha kuwa kila mtumishi anawajibika ipasavyo kwenye jukumu lake alilopangiwa na kuwataka Maafisa Utumishi kusimamia wajibu wao wa kazi ili dhamira ya serikasli iweze kufikiwa.
Aidha amewataka Maafisa Utumishi hao kufanya kazi kwa mashirikiano na kupeana taarifa miongoni mwao sambamba na kubadilisha uzowefu huku akiahidi kuwa Afisi yake inawapatia kila aina ya mahitaji wanayoyataka kwa dhamira ya kuwasimamia wafanyakazi wao wanawaongoza katika maeneo yao ya kazi
Akizungumzia kuhusu suala la umuhimu wa mafunzo kwa Maafisa Utumishi Ndugu Mohamed amewaahidi Maafisa hao kuwapatia taaluma stahiki zitakazoendana na utendani wa kazi zao kwa kuzingatia mabadiliko ya Teknolojia nchini.
Kwa upande wao Maafisa hao wameomba kupatiwa mafunzo ya Ujengaji Uwezo sanjari na ziara za mafunzo ndani na nje ya nchi ili kuongeza ujuzi, elimu na taaluma ya kazi zao
Aidha wameushukuru uongozi wa Afisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi kwa jitihada zake za kuzipatia ufumbuzi changamoto mbalimbali zinazowakabili katika maeneo yao ya kazi. Kikao kazi hicho kiliwahusisha Maafisa Utumishi kutoka Baraza la Manispaa Mjini, Baraza la Manispaa Magharibi “A”, Baraza la Manispaa Magharibi “B” Pamoja na Maafisa Utumishi wa Wilaya zote zilizomo ndani ya Mkoa wa Mjini Magharibi