OFISI YA RAIS
TAWALA ZA MIKOA NA IDARA MAALUM ZA SMZ

OFISI YA MKUU WA MKOA MJINI MAGHARIBI

Home>>Habari>>Mpango wa kudhibiti Malaria 2023 – 2028 waanza
HabariHabari Mpya

Mpango wa kudhibiti Malaria 2023 – 2028 waanza

Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Mhe.Idrissa Kitwana Mustafa amesema mashirikiano ya wadau mbali mbali ni muhimu katika kufanikisha mpango wa miaka mitano wa kutokomeza malaria hapa Zanzibar.

Amesema hayo alipokuwa akifungua mkutano wa kutoa uelewa juu ya hali ya ongezeko la malaria  pamoja na kuweka mikakati ya kupambana na maradhi hayo uliyofanyika katika hoteli ya Golden Tulip Kiembe Samaki.

Amesema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ina dhamira ya dhati ya kutokomeza maradhi hayo hapa nchini, hata hivyo lengo hilo halitaweza hafikiwa ikiwa itaachiwa Wizara ya Afya pekee kulisimamia.

Mkuu wa Mkoa ameipongeza Wizara ya Afya  kwa kuja na mpango mkakati wa miaka mitano wa kuthibiti maambukizi  ya  malaria nchini ambao utashirikisha wadau mbali mbali na kusema kuwa Mkoa wake utatoa kila aina ya mashirikiano ili kuona mpango  huo unafanikiwa.

Vilevile ameishukuru pia Wizara ya Afya kwa kuanza utekelezaji wa mpango huo kwenye Mkoa wake kwa ugawaji wa vyandarua na kusema kuwa zaidi ya vyandarua laki mbili (213,564) tayari vimeshagaiwa huku zoezi hilo  kitarajiwa kuendelea ili kukamilisha idadi ya vyandarua vilivyokusudiwa kutolewa katika Mkoa Mjini Magharibi.

Aidha Mkuu huyo wa Mkoa amewataka wananchi kuendelea kuchukua tahadhari ya kujikinga na mambo yanayopelekea maambukizi ya maradhi ya malaria ili kupunguza ongezeko la maradhi hayo.

Amesema bado maradhi hayo ni hatarishi kwenye Mkoa huo kutokana na idadi kubwa ya wageni wanaoingia kutoka sehemu mbali mbali ndani na nje ya Zanzibar.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kinga kutoka Wizara ya Afya Dkt. Slim Salum Slim amesema lengo la Serikali kuweka  mpango huo ulioanza utekelezaji wake mwezi Juni mwaka huu hadi 2028 ni kuhakikisha inadhibiti kabisa maambukizi ya malaria.

Akitoa mada kuhusu hali ya malaria Zanzibar, Afisa ufuatiliaji wa Kitengo cha Kudhibiti Malaria Zanzibar Raya Ibrahim amesema takwimu zinaonesha kuwa asilimia 79 ya kesi za malaria zinatokana na wageni  walioingia kutoka nje ya Zanzibar huku asilimia 21 ya wagonjwa ni maambukizi ya ndani.

Amesema vijana wenye umri wa miaka 15 na zaidi ndio waathirika wakubwa tofauri na miaka ya nyuma ambapo watoto chini ya miaka 5 ndio waliyokuwa wakiathirika zaidi na ugonjwa wa malaria.

Wakichangia juu ya mikakati ya kudhibiti maradhi hayo washiriki wa mkutano huo wamesema bado muamko wa jamii  kujikinga na malaria ni mdogo na kuishauri Wizara ya Afya kuelekeza nguvu zaidi kuielimisha jamii kujikinga na maradhi hayo.