Waziri wa Habari Vijana Utamaduni na Michezo Mhe. Tabia Maulid Mwita amezindua rasmi maegesho ya gari yaliyojengwa na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF), eneo la Michenzani Mall.
Akihutubia mara baada ya uzinduzi huo Waziri Tabia amewataka ZSSF, Manispaa na Mkoa kuhakikisha eneo hilo lililojengwa kwa ajili ya maegesho ya gari na vyombo vya maringi mawili linatumika badala ya watu kuegesha vyombo vyao barabarani.
Ameipongeza ZSSF kwa ujenzi wa mradi huo ambao amesema utapunguza tatizo la maegesho katika jengo la Michenzani Mall na kuwataka kufikiria kujenga maegesho zaidi katika maeneo mbali mbali ya Mji.
Waziri Tabia ameitaka Wizara ya Nchi (OR) Fedha na Mipango kuendelea kushirikiana na ZSSF ili kutekeleza miradi mingine zaidi ambayo itarahisisha upatikanaji wa huduma kwa wananchi wa Mkoa Mjini Magharibi na Zanzibar kwa ujumla
Naye Mhe. Sabiha Filifil Thani Mjumbe wa Kamati ya Uchumi ya Baraza la Wawakilishi akizungumza kwa niaba ya Kamati hiyo ameushauri Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar kutekeleza miradi yenye tija ili Mfuko huo uweze kujiendesha na kulipa mafao ya wastaafu.
Awali akizungumzia mradi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa ZSSF Nassor Shaaban Ameir amesema maegesho hayo yana uwezo wa kuegesha gari sabini na tisa, vyombo vya maringi mawili, eneo kwa ajili ya watu wenye mahitaji maalum na milango sita ya huduma za ATM.
Viongozi, wafanya kazi wa taasisi mbali mbali za Serikali pamoja na wananchi walihudhuria hafla hiyo ikiwa moja ya matukio ya Maadhimisho ya Kutimiza Miaka 59 ya Mapinduzi ya Zanzibar ambayo kilele chake kitafikia tarehe 12 Januari.