Watumishi wa Umma wametakiwa kufuata ipasavyo maadili ya kazi zao katika kutekeleza majukumu waliyopangiwa.
Akizungumza na wafanyakazi katika ziara ya kushtukiza Ofisi ya Baraza la Manispaa Magharibi B, Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Mhe. Idrissa Kitwana Mustafa amesema suala la wafanyakazi kuwa waadilifu ni muhimu katika kuleta ufanisi na kufikia malengo yaliyowekwa na sekta husika.
Aidha amekemea tabia ya baadhi wa watumishi wa Baraza hilo kutokwepo katika maeneo yao ya kazi kwa visingizio mbali mbali na kusema kuwa vitendo hivyo vinarudisha nyuma juhudi za Serikali zinazowataka watumishi kuwahudumia wananachi.
Akielezea kuhusu wajibu wa mtumishi, Mhe. Idrissa ameeleza kutoridhishwa na mahudhurio ya wafanyakazi katika Ofisi hiyo na kuwataka kuacha kufanya kazi kimazoea.
Mkuu wa Mkoa ameawaagiza maafisa utumishi, wakuu wa vitengo na idara kuwasimamia wafanyakazi waliopo chini yao na kuwachukulia hatua kwa mujibu wa taratibu za kiutumishi kwa wale wanaokwenda kinyume na taratibu zao za kazi.
Akizungumza kwa niaba ya watendaji, Afisa Utumishi Ofisi ya Baraza la Manispaa Magharibi B Warda Said Masoud ameahidi kuwa watayafanyiakazi maagizo ya Mkuu wa Mkoa ili kuhakikisha kila mfanyakazi anatekeleza majukumu yake kikamilifu.