Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Nchini (TASAF), kwa upande wa Unguja umetakiwa kuhakikisha unasimamia vyema miradi ya maendeleo itakayotekelezwa katika awamu ya tatu ya mradi huo.
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi wa TASAF Unguja Mhe. Idrissa Kitwana Mustafa katika kikao cha Kamati hiyo kilichokutana Afisi ya Mkuu wa Mkoa Vuga kujadili masuala mbali mbali ikiwemo kuidhinisha miradi itakavyotekelezwa na TASAF kwa mikoa mitatu ya Unguja.
Amesema kwamba kamati yake itafatilia kwa karibu utekelezaji wa miradi hiyo ili kuona inatekelezwa kwa ubora, kiwango kinachotakiwa na kukamilika kwa muda uliopangwa.
Sambamba na hilo Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi wa TASAF Unguja ametaka fedha zitakazotengwa kwa ajili ya miradi hiyo zitumike vizuri ili miradi hiyo iweze kukamilika na kuleta tija kwa wananchi.
Aidha amesema kwamba Mikoa pamoja na Wilaya zote kwa upande wa Unguja wataendelea kushirikiana na watendaji wa TASAF Zanzibar katika utekelezaji wa miradi mbali mbali.
Naye Mratibu wa Tasaf Unguja Makame Ali Haji amesema kwamba jumla ya miradi mitatu itanufaika katika awamu hiyo ikiwemo ukarabati wa Hospitali ya macho Mkele, Skuli ya maandalizi Mzalendo na ujenzi wa ukumbi wa mitihani Skuli ya Potoa.