Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Mhe. Idrissa Kitwana Mustafa amekutana na kufanya mazungumzo na Jumuia ya Kupiga vita Rushwa na Uhujumu Uchumi Zanzibar (JUKURUZA), walipofika ofisini kwake Vuga kujitambusha.
Mkuu wa Mkoa amewapongeza viongozi wa Jumuia hiyo kwa kuamua kuunda chombo hicho chenye azma ya kuiunga mkono Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika mapambano dhidi ya rushwa na uhujumu uchumi.
Ameitaka Jumuia hiyo kuhakikisha kuwa wanasimamia dhamira ya kuundwa kwa chombo hicho ili malengo waliyojiwekea waweze kuyafikia .
Mhe. Idrissa amewatanabahisha kuwa kumekuwepo na mtindo kwa baadhi ya watu kuanzisha Jumuia kwa nia njema ya kuisaidia jamii lakini hatimaye huacha malengo ya kuanzishwa kwa Jumuia hizo na kujiingiza katika mambo ambayo yanakiuka sheria na taratibu za nchi.
Mwenyekiti wa JUKURUZA Khalfan Ali Faki amemueleza Mkuu wa Mkoa kuwa dhamira ya kuanzishwa kwa Jumuia hiyo ni kupiga vita vitendo vya rushwa na uhujumu uchumi katika ngazi mbali mbali na ameomba kupatiwa mashirikiano ya Mkoa, Wilaya na Shehia katika kutekeleza shughuli zao.