OFISI YA RAIS
TAWALA ZA MIKOA NA IDARA MAALUM ZA SMZ

OFISI YA MKUU WA MKOA MJINI MAGHARIBI

Home>>Habari>>RC ahimiza usafi baraza la manispaa Mjini
HabariHabari Mpya

RC ahimiza usafi baraza la manispaa Mjini

Baraza la Manispaa Mjini pamoja na Madiwani wa Wadi mbali mbali ziliomo katika Wilaya ya Mjini wametakiwa kuondoa muhali katika kusimamia suala la usafi wa Mji katika Manispaa hiyo. Agizo hilo limetolewa na Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Idrissa Kiwana Mustafa wakati alipofanya ziara yake kufatilia hali ya usafi katika barabara na maduka yaliopo barabara kuu itokayo Mombasa hadi Mwanakwerekwe.

Amesema bado kuna wafanyabiashara hawazingatii maelekezo wanayopewa na Serikali katika kuhakikisha wanaweka usafi katika maeneo yao ya biashara hali inayochangia uchafuzi wa mazingira kwenye barabarara kuu. Amelitaka Baraza la Manispaa kuanzia sasa kutumia kanuni zao za faini za papo kwa papo na hata kuwafutia leseni za biashara wenye maduka wasioweka mazingira safi mbele ya maduka yao ili kuthibiti vitendo vya uharibifu wa mazingira kwenye maeneo ya barabara kuu.

Mkuu wa Mkoa amelitaka Baraza hilo pia kuhakikisha kuwa maeneo ya hifadhi ya barabara yanakuwa wazi na hayatumiwi na wafanyabishara kuweka bidhaa zao kwani kufanya hivyo kunawazuia watembea kwa miguu na wananchi wengine kutumia maeneo hayo.

Aidha Mkuu wa Mkoa amesema bado wasimamizi wa usafi katika Manispaa hiyo hawatekelezi wajibu wao ipasavyo, hivyo amelitaka Baraza la Manispaa na Madiwani kushirikiana kwa pamoja katika kulisimamia suala la usafi ndani ya Wilaya ya Mjini.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Mjini Rashid Simai Msaraka amewataka wamiliki wa maduka yaliyopo pembezoni mwa barabara kuu mbali mbali ndani ya Wilaya hiyo kuyapaka rangi na kuweka mabango ya majina ya maduka yao ili kuwa na muonekano mzuri.