Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdalla amewashukuru wananchi wa Mkoa Mjini Magharibi kwa kuendelea kumuunga mkono Rais wa Zanzibar katika juhudi zake za kuwaletea maendeleo wananchi.
Shukurani hizo amezitoa wakati akisalimiana na wananchi katika maeneo mbali mbali akiwa katika ziara yake Wilaya ya Magharibi B kukagua ujenzi wa miradi ya maendeleo inayojengwa kupitia fedha za UVIKO 19. Amesema kitendo chao cha kujitokeza kwenye kila mradi anaotembelea kinaipa moyo Serikali katika utekelezaji wa miradi hiyo ya maendeleo.
Aidha Makamu wa Pili wa Rais amewataka vijana kusoma kwa bidii ili waje kufanyakazi katika miradi hiyo na kusema kuwa wakati itakapokamilika itaongeza fursa ya ajira ikiwemo sekta ya afya na elimu.
Makamu wa Pili wa Rais Ameitaka pia Kampuni ya CRJE kuongeza wafanyakazi ili kazi za ujenzi wa Hospitali za Wilaya ziende kwa kasi na kumalizika kwa wakati. Amesema hakuna sababu ya kuchelewa kwa miradi hiyo kwa kisingizio cha uchache wa vibarua ilhali vifaa vya na fedha za ujenzi zipo. Kauli hiyo imekuja kufuatia taarifa iliyotolewa na Wizara ya Afya kuwa ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Magharibi B ujenzi wake uko nyuma ya wakati.
Naye Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa Magharibi Mohammed Rajab amesema Chama kinaridhishwa na utekelezaji wa ilani katika Mkoa wake. Kwa upande wao wananchi wa Wilaya hiyo wamemshukuru Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dkt. Hussein Ali Mwinyi kwa ujenzi wa miradi hiyo.
Jumla ya madarasa 54, masoko ya wajasiriamali na Hospitali ya Wilaya inajengwa katika Wilaya ya Magharibi B kupitia fedha hizo.