Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Idrissa Kitwana Mustafa amewahimiza viongozi wa mabaraza ya vijana taifa, mkoa, wilaya na shehia kupanga mikakati madhubuti ili kuhakikisha vijana wanaendelea kulindwa dhidi ya maambukizi ya virusi vya ukimwi.
Ametoa rai hiyo alipokuwa akifungua kongamano la kujadili Ukimwi na vijana lililoandaliwa na Tume ya Ukimwi Zanzibar (ZAC), ikiwa katika kuelekea maadhimisho ya siku ya Ukimwi Duniani tarehe 1 Disemba ya kila mwaka.
Akifungua kongamano hilo katika ukumbi wa Idrissa Abdul Wakil, Mkuu wa Mkoa amesema pamoja na juhudi mbali mbali zinazochukuliwa kuwaelimisha vijana, asilimia 50 ya watu wanaogundulika na Ukimwi nchini ni vijana wenye umri kati ya miaka 15-24, hivyo ni muhimu kwa taasisi za umma, binafsi na makundi ya kijamii kushiriki kikamilifu katika kupambana na maradhi hayo ili vijana waweze kubaki salama.
Idrissa ametanabahisha kuwa licha ya mafanikio yaliyopatikana katika kuyadhibiti maradhi hayo na kubaki chini ya asilimia 1 tangu yalipoingia nchini mwaka 1986, bodo kuna haja ya kuongeza nguvu ili kuweza kufikia lengo la ulimwengu la kumaliza UKIMWI ifikapo 2030.
Sambamba na hayo Mkuu wa Mkoa ameyashukuru mashirika ya maendeleo yanayosaidia mapambano dhidi ya UKIMWI ikiwemo UNAIDS,UNFPA,UNICEF na AMREF na kusema kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na kufanya nao kazi kwa pamoja na mashirika hayo.
Mkurugenzi wa Tume ya Ukimwi Zanzibar, Ahmed Mohamed Khatib amewataka vijana kujiepusha na mambo yanayowapelekea kupata maambukizi ya VVU.
Ametaja baadhi ya vitendo hivyo ni kuwa na mahusiano na watu wenye umri mkubwa, kujiingiza kwenye uhusiano kwenye umri mdogo, mahusiano zaidi ya mtu mmoja, tamaa ya vitu vya vyamani na kutojitambua kuwa wapo katika mazingira hatarishi ya kuweza kupata UKIMWI.
Kwa upande wao vijana waliochangia katika kongamano hilo wamesema baadhi ya vijana wametumbukia katika vitendo hivyo kutokana na baadhi ya wazazi kutokuwa karibu na watoto wao na kuwapa ushauri.
Kadhalika wamewashauri vijana wenzao kujitambua, kuacha tamaa na kutaka maendeleo ya haraka haraka.
Mada tatu ziliwasilishwa katika kongamano hilo ikiwemo Hali halisi ya UKIMWI Zanzibar, Umuhimu wa Mabaraza ya Vijana na Fursa zilizopo Wakala wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi.