Fainali ya kombe la Mapinduzi Cup kwa timu za Wizara Mashirika na Taasisi za SMZ iliyokuwa ipigwe jana kati ya Tawala na Hospitali ya Kivunge katika uwanja wa Aman imeahirika baada ya golikipa wa Tawala Bakari Juma Moh’d kuugua muda mchache kabla ya mchezo kuanza.
Nahodha wa timu ya Tawala Said Kombo Ali alieleza kuwa hadi wanafika uwanjani hakukua na mchezaji yoyote aliyekuwa majeruhi au kusumbuliwa na maradhi, hata hivyo mara tu baada ya kupasha moto viungo na kurudi vyumba vya wachezaji ghafla golikipa wao alianza kuugua na kuzungumza maneno yasiyoeleweka.
Kufuatia tukio hilo wachezaji wa Tawala walipata taharuki na hivyo kushindwa kuingia uwanjani kuendelea na mchezo.
Kutokana na mkasa huo kamati inayosimamia mashindano hayo iliamua kuahirisha mchezo huo na hadi tunaondoka uwanjani hakukutolewa taarifa yoyote juu ya mchezo huo kupigwa siku nyengine.