OFISI YA RAIS
TAWALA ZA MIKOA NA IDARA MAALUM ZA SMZ

OFISI YA MKUU WA MKOA MJINI MAGHARIBI

Home>>Habari>>ACP Richard afichua Wahalifu  na kukamata  Bastola
HabariHabari Mpya

ACP Richard afichua Wahalifu  na kukamata  Bastola

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi  linamshikilia Ndugu Khelef Khamis Abeid mwenye umri wa miaka kumi na nane (18) Mkaazi wa Bububu kwa kupatikana na  Bastola aina ya Bareta yenye risali tano katika maeneo ya Forodhani.

Akitoa taarifa kwa  Waandishi wa Habari huko Afisini kwake Muembe Madema Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi ACP Richard Thadei Mchomvi amesema kuwa katika operesheni wake wa  kawaida Jeshi hilo limefanikiwa kumkamata Mtuhumiwa  huyo na baadae kuendelea kufanya upelelezi nyumbani kwake na kufanikiwa kupata risasi moja ndani ya chumba anacholala.

Amesema kuwa katika hatua ya mahojiano ya awali Mtuhumiwa huyo amekiri kumiliki  Bastola kinyume na utaratibu, hali iliyopelekea kuzidi kuendelea na  upelelezi na mara baada ya upelelezi huo kukamilika ipasavyo Mtuhumiwa huyo atafikishwa Mahakamani kwa ajili ya kujibu shtaka linalomkabili.

Katika hatua nyengine Jeshi la Polisi Mkoa wa Mjini Mgharibi  limefanikiwa kuwakamata watu 15 wa makosa tofati ikiwemo Unyang’anyi, Wizi, Uporaji, Utapeli, Wizi baada ya kuaminiwa, kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu, shambulio la hatari na Ubakaji.

ACP Richard amazitaja mali walizokamatwa nazo watuhumiwa hao  kuwa ni  Simu 58, Laptop 2, TV 2, Honda aina ya ADV yenye namba za usajili Z903 LR, Madumu 55 ya mafuta aina ya Diseil, Mikoba ya Kina mama, baiskeli aina ya Sehewa pamoja na  nguo za Daktari ambazo alikamatwa nazo Mtuhumiwa katika Hospitali ya Mnazi Mmoja akiwa amevaa na kupita  katika Vitanda vya wagonjwa waliolazwa na kuwaibia vitu vyao.

Amesema watuhumiwa hao kesi zao zinaendelea kusikilizwa mahakamani kwa mashirikiano ya karibu kati ya Jeshi la Polisi, Afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka Mahakama pamoja na Vyuo vya Mafunzo. Hata hivyo, Kamanda Richard ametoa wito kwa Wananchi kuwacha tabia ya umuhali na kuhakikisha kuwa kesi hizo zinatolewa ushahidi ili hatua za kisheria ziweze kutekelezeka ipasavyo.

Aidha amekemea tabia ya baadhi ya watu kupitisha suluhu wenyewe kwa wenyewe huku kesi ikiwa inasubiri mlalamikaji jambo ambalo linasababisha wahalifu kushinda kesi mahakamani na kuwafanya watuhumiwa hao kuwa huru kutokana na kukosekana Ushahidi, “Wananchi waache tabia ya muhali tumebaini kuwa watuhumiwa wengi wa makosa ndio wale wale na makosa yao yanajirejea lakini kama wangelichukuliwa hatua tusingekua na watuhumiwa kabisa” alisema.

Aidha amesema Jeshi la Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi linaendelea kudumisha Usalama wa Raia na Mali zao kwa kufanya Doria  na Misako ya kuwakamata watuhumiwa wanaotenda uhalifu.

Kadhalika Jeshi la Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi linapenda kuwafahamisha wananchi kwamba hali ya usalama katika Mkoa wake ipo vizuri kutokana na ushirikiano mzuri uliopo kati ya wananchi na vyombo vyengine vya ulinzi na usalama.