Shamrashamra za Maadhimisho ya Miaka 60 ya Mapinduzi ya Zanzibar zimeendelea katika Mkoa Mjini Magharibi ambapo Rais Mstaafu wa Zanzibar Dkt. Amani Abeid Karume amefungua Hospitali ya Wilaya ya Magharibi ‘B’ iliopo Mwanakwere Jitimai.
Katika hafla hiyo iliyohudhuriwa pia na viongozi mbali mbali wa Serikali, vyama vya siasa, watendaji wa Wizara ya Afya na wananchi, Dkt. Amani mara tu alipowasili aliweka jiwe la ufunguzi, alikata utepe pamoja kukagua kukagua na Hospitali hiyo mpya.
Akihutubia wananchi waliohudhuria shughuli hiyo Rais Mstaafu wa Zanzibar Awamu ya Sita amempongeza Dkt.Hussein Ali Mwinyi kwa juhudi kubwa anazochukua katika ujenzi wa miundo mbinu mbali mbali.
Amesema hatua hiyo inadhihirisha namna Serikali ya Awamu ya Nane inavyoendelea kutekeleza dhamira ya Mapinduzi ya Zanzibar ya Januari 12 1964 ya kuwapatia wananchi huduma zote muhimu ikiwemo afya.
Kwa upande mwengine Dkt. Karume aligusia pia umuhimu wa wananchi kuchukua kinga dhidi ya maradhi mbali mbali hasa maleria ambapo hivi sasa maambukizi yake yanaonekana kuongezeka kwa baadhi ya Shehia za Mkoa Mjini Magharibi.
Amesema wananchi wanawajibu wa kufuata ushauri unaotolewa na wataalamu katika kujikinga na maradhi hayo na kusema kuwa hatua hiyo itaipunguzia mzigo Serikali kutumia fedha nyingi kwa ajili ya kutoa matibabu.
Waziri wa Afya Nassor Ahmed Mazurui amesema Zanzibar ikiwa inatimiza miaka 60 tangu Mapinduzi, Serikali inaendelea kutoa huduma za matibabu bure kwa wananchi wote.
Akitoa salamu za wananchi wa Mkoa Mjini Magharibi kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya ya Magharibi ‘B’ Hamida Mussa Khamis amesema wananchi wa Mkoa huo wanathamini sana hatua iliyochukuliwa na Serikali ya kuwasogezea karibu Hospitali ambazo wanaweza kupata huduma mbali mbali za matibabu.
Amesema Mkoa utahakikisha Hospitali hizo zinatunzwa na hatua za kisheria zitachukuliwa kwa wale watakaojaribu kuharibu majengo hayo.
Hospitali ya Wilaya ya Magharibi ‘B’ imeanza kutoa huduma Septemba mosi 2023 na mpaka inafunguliwa rasmi ishahudumia wagonjwa 17,256.