OFISI YA RAIS
TAWALA ZA MIKOA NA IDARA MAALUM ZA SMZ

OFISI YA MKUU WA MKOA MJINI MAGHARIBI

Home>>Habari>>Wachukulieni  hatua wafanyakazi wasiowajibika. RAS
HabariHabari Mpya

Wachukulieni  hatua wafanyakazi wasiowajibika. RAS

Uongozi wa Wilaya na Baraza la Manispaa Magharibi ‘B’ umetakiwa kutosita kuchukua hatua za kinidhamu dhidi ya wafanyakazi wasiowajibika.

Agizo hilo limetolewa na Katibu Tawala Mkoa Mjini Magharibi Moh’d Ali Abdalla katika kikao kilichoshirikisha viongozi na wafanyakazi wa Wilaya na Manispaa hiyo kilichozungumzia masuala mbali mbali ya kiutendaji.

Amesema endapo watendaji na wafanyakazi watashindwa kutimiza majukumu yao kama walivyopangiwa  wachukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria, miongozo na taratibu za kiutumishi bila ya kumuonea mtu.

Sambamba na hayo Katibu Tawala amewaagiza Wakuu wa Vitengo kwa upande wa maegesho ya vyombo vya moto na masoko kuhakikisha wanawasimamia vilivyo wafanyakazi waliyo chini yao kwa vile bado mapato yatokanayo na vyanzo hivyo yamekuwa yakivuja.

Kwa upande mwengine Moh’d amesema hali ya usafi kwenye barabara kuu ndani ya Manispaa hiyo bado sio ya kuridhisha hivyo amataka  kuanzia sasa  barabara zote kuu ziwe zikisafishwa mara mbili kwa siku badala ya utaratibu uliyozoeleka wa kusafisha  wakati wa asubuhi.

Naye Mstahiki Meya wa Manispaa Magharibi ‘B’ Khamis Hassan Haji  amesema baadhi ya wafanyakazi  hawatekelezi majukumu yao na wamekuwa wakifanya kazi kimazoea. Amewataka kubadilika kiutendaji ili Manispaa hiyo iweze kufikia malengo waliyojiwekea.

Awali wafanyakazi hao walizitataja changamoto mbali mbali zinazokwamisha ufanisi katika utendaji wao wa kazi ikiwemo uhaba wa vitendea kazi, malipo ya posho la masaa ya ziada ya kazi na kukosa mashirikiano ya jamii katika suala zima la usafi kwenye maeneo yao.

Kikao hicho kilifanyika katika ukumbi wa mikutano Manispaa Magharibi ‘B’ kilihudhuriwa pia na Mkuu wa Wilaya hiyo Hamida Mussa Khamis, Mkurugenzi wa Manispaa Khadija Said pamoja na wafanyakazi wa  Vitengo mbali mbali.