Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Mhe. Idrissa Kitwana Mustafa amewahimiza madereva wa Boda boda kuhakikisha wanavaa sare na beji zitakazowatambulisha ili watumiaji wa usafiri huo waweze kuwatambua madereva waliosajiliwa kuifanya kazi hiyo.
Mkuu wa Mkoa ametoa wito huo katika kikao chake na Uongozi wa Jumuia ya Waendesha Bodaboda hapo Afisini kwake Vuga.
Amesema kutokana na ongezeko la vyombo hivyo kuna umuhimu mkubwa wa madereva hao kuvaa sare pamoja na beji ili jamii iweze kuwatambua na kuhakikisha usalama wao pale wanapotumia usafiri huo.
Aidha amesema amewataka madereva wa bada boda kufuata sheria na taratibu zilizopo kwani takwimu zinaonesha idadi kubwa ya ajali na vitendo vya kihalifu vinatokana madereva wa vyombo hivyo.
Katika kudhibiti vitendo hivyo Mkuu wa Mkoa amelitaka Jeshi la Polisi Mkoa Mjini Magharibi kuendesha operesheni za mara kwa mara za kuwakamata madereva wanaoendesha vyombo hivyo bila leseni na wanaovunja sheria za barabarani.
Kwa upande mwengine Idrissa ameutaka uongozi wa madereva wa boda boda kuwashajiisha wanachama wao kujiunga na mafunzo yanayotolewa na Idara ya Mawasiliano kwa madereva wa boda boda.
Amefahamisha kuwa Serikali imepunguza malipo ya mafunzo hayo kutoka shilingi laki mbili hadi elfu arubaini kwa lengo la kutaka madereva wote kupata mafunzo hayo na kuwataka kuitumia vizuri fursa hiyo.
Mkuu wa Mkoa amesisitiza kuwa Serikali imerasimisha vyombo hivyo kuwa usafiri rasmi wa kubeba abiria, hivyo kuna umuhimu wa kupata mafunzo hayo ili waweza kufanya kazi zao kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizowekwa.
Kadhalika amewashauri kuwa na siku maalumu itakayowakutanisha madereva hao kwa lengo la kuzungumzia changamoto zinazowakabili, mafanikio yao pamoja na njia za kuboresha usafiri huo.
Nae Kamanda wa Polisi Mkoa Mjini Magharibi Richard Mchomvu ameahidi kuyafanyia kazi maagizo ya Mkuu wa Mkoa na kuwataka madereva wa boda boda kufuata sheria ili kuepuka kuchukuliwa hatua za kisheria.
Uongozi wa Jumuiya ya Madereva wa Bodaboda wameiomba Serikali ya Mkoa kuwathibiti waendesha boda boda wasiyosajiliwa kwa vile wamekuwa wakiichafua kazi hyo na kujihusidha na matendo ya uhalifu.
Kati ya boba boda 2119 zilizosajiliwa, madereva 911 sawa na asilimia 4.6 ndio waliokiswapata mafunzo kufanya kazi hiyo.