OFISI YA RAIS
TAWALA ZA MIKOA NA IDARA MAALUM ZA SMZ

OFISI YA MKUU WA MKOA MJINI MAGHARIBI

Home>>Habari>>Mbinu mpya za usimamizi fedha ni kiini cha uwajibikaji – RC Kitwana
Habari

Mbinu mpya za usimamizi fedha ni kiini cha uwajibikaji – RC Kitwana

Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Mhe Idrissa Kitwana Mustafa amewataka watendani wa mashirika ya Umma na taasisi za kifedha kuwa na mbinu bora za usimamizi mzuri wa kazi zao ili kuleta ufanisi katika kazi.

Mkuu wa Mkoa ameyasema hayo huko Maisara katika ukumbi wa Afisi za ZURA wakati akifungua mafunzo ya usimamizi wa mashirika ya Umma yaliyowashirikisha maafisa wa sekta mbali mbali za serikali zinazohusiana na masuala ya kifedha.

Amesema mafunzo hayo yatawasaidia kuwajengea uwezo hasa kwa kuzingatia usimamizi wa mashirika ya kiserikali katika kutambua na kupunguza hatari za kifedha pamoja na kutoa mbinu za jumla za uchambuzi juu ya masuala ya kifedha.

Aidha amesema mafanikio ya ujumla yatakayopatikana yatatokana na huduma bora zitakazotolewa na watendaji, hata hivyo amesema hatua hiyo inahitaji uwajibikaji na uwadilifu kwa wafanyakazi na watendaji ili kuhakikisha kuwa shughuli za kila siku zinafanyika vizuri.

Mheshimiwa Kitwana ameongeza kuwa mafunzo hayo yataongeza kuleta maslahi mapana kwa nchi na kuwa yenye mnasaba kwa jamii jambo ambalo litawajenga kujua baadhi ya taarifa hususan katika suala zima la muongozo wa bajeti na waraka.

Nae Mkuu wa usimamizi wa mashirika na uwekezaji Zanzibar Mussa Ali Juma amesema elimu inayotolewa kwa Maafisa hao italenga katika kuleta tathmini kwa taasisi juu ya matumizi ya kifedha

Vile vile amesema wanaimani kubwa kwa taasisi hizo juu ya mafunzo hayo kwa kuweza kujitathmini kifedha kuzalisha zaidi, kupata mtaji mzuri, kuwa na uwezo wa kuandaa bajeti zitakazowasaidia katika mipango yao pamoja na kujitathmini kupitia mikataba wanayopatiwa kila ifikapo mwisho wa mwaka

Mafunzo hayo yaliyoandaliwa na Afisi ya Msajili wa hazina yenye lengo la kufahamu muongozo wa bajeti na suala zima la waraka yamehusisha mada mbalimbali ikiwemo usimamizi wa rasilimali watu, haki na wajibu wa mfanyakazi pamoja na maadili ya mtumishi wa Umma.