Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mhe. Hemed Suleimn Abdalla ameviagiza Vikosi vya SMZ vilivyokabidhiwa kazi ya ujenzi wa masoko katika Mkoa Mjini Magharibi kuongeza kasi ujenzi wa miradi hiyo iweze kukamilika ndani ya wakati uliyokusudiwa.
Agizo hilo amelitoa wakati alipofanya ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa Soko la Mwanakwereke, Jumbi na Chuini akiwa pamoja na Viongozi na mbali mbali Serikali.
Mhe. Hemed ameeleza kuridhishwa na hatua iliyofikiwa ya ujenzi wa masoko hayo ndani ya mwezi mmoja tangu alipofanya ziara yake mwezi mmoja uliopita na kuwataka waongeze juhudi ili pale atakapotembelea tena mwezi ujao kuwe na mabadiliko makubwa ya ujenzi huo.
Aidha Makamu wa Pili wa Rais amewapongeza wajenzi Kikosi cha Chuo cha Mafunzo, Jeshi la Kujenga Uchumi (JKU) na Kikosi cha Zima moto na Uokozi kwa hatua nzuri waliyofikia kwenye miradi hiyo.
Amesisitiza kuwa anamatarajio miradi hiyo itakamilika mapema ili kuiwezesha Serikali kuendelea kutekeleza miradi mengine mikubwa ya maendeleo.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Mhe. Idrissa KItwana Mustafa amesema ujenzi wa masoko hayo unakwenda kutoa nafasi za ajira zaidi ya elfu nne kwa wananchi wa Mkoa wake.
Naye Katibu Mwenezi wa Chama cha Mapinduzi Zanzibar Khamis Mbeto amemweleza Makamu wa Pili wa Rais kuwa kama wasimamizi wa Ilani ya CCM wanaridhishwa na maendeleo ya ujenzi wa miradi ya maendeleo inayoendelea kutekelezwa na Serikali ya Awamu ya Nane chini ya uongozi wa Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi.