Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Mhe. Idrissa Kitwana Mustafa amewashukuru mashekh kwa namna walivyoutumia mwezi Mtukufu wa Ramadhani kwa kutoa elimu ya dini pamoja na kugusia mambo ya kijamii katika darsa na matukio mbali mbali yaliyofanyika ndani ya mwezi huo.
Ametoa shukurani hizo wakati akizungumza na Mashekh na Maimamu wa misikiti mbali mbali hapo afisini kwake Vuga.
Ameeleza kuwa Serikali ya Mkoa imefarajika na namna viongozi hao mbali ya kutoa elimu ya dini vilevile wameweza kuiasa jamii kuachana na mambo ya udhalilishaji na yanayoenda kinyume na silka na utamaduni wa wazanzibari.
Aidha amewaomba viongozi hao kuendelea kuikumbusha jamii juu ya umuhimu wa kutenda mambo mema, umoja na mshikamano miongoni mwa wananchi.
Mkuu wa Mkoa ameishukuru pia Ofisi ya Mufti kwa kusimamia vyema shughuli mbali mbali za kidini yakiwemo mashindano ya kuhifadhi Qur-an, kutoa sadaka na darsa yaliyofanyika ndani ya Mkoa huo katika mwezi Mtukufu wa Ramadhani.
Naye Katibu Mtendaji wa Ofisi ya Mufti Mkuu Zanzibar Shekh Khalid Ali Mfaume amemueleza Mkuu wa Mkoa kuwa Ofisi yake itaendelea kusimamia shughuli za kidini nchini ili kuhakikisha jamii inaendelea kuwa kitu kimoja.