Mkuu wa mkoa wa Mjini Magharibi Mhe. Hassan Khatib Hassan amezitaka familia zinazoishi karibu na shimo linalochimbwa kifusi katika shehia ya Mtoni Chemchem kuhama mara moja ili kunusuru maisha yao kutokana na uharibifu wa mazingira ya eneo hilo.
Mkuu wa mkoa ametoa agizo hilo katika ziara aliyoifanya kungalia athari zilizijitokeza kutokana na uchimbaji wa kifusi kwenye eneo hilo ambao umeziweka nyumba za familia hizo katika hatari ya maisha yao na mali zao.
Amesema kitendo cha wananchi hao kuendelaa kuishi katika nyumba hizo ni hatari na kuutaka uongozi wa wilaya ya Magharibi ‘A’ na manispaa ya wilaya hiyo kusimamia maamuzi hayo sambamba na kuzuia uchimbaji wa kifusi katika eneo hilo ili kuepusha madhara zaidi.
“Mkuu wa wilaya na Mkurugenzi maamuzi mliyoyachukua ya kuwazuwia wananchi kuendelea kuishi katika nyumba hizi ninauunga mkono kwani usalama wa maisha yao ni jambo la muhimu kwetu kama serikali lakini ipo haja ya kuwekwa mipaka hasa ni nyumba gani ziendelee kutumika kwa makaazi,”alisema Mhe. Hassan.
Aidha Mkuu wa mkoa huyo amesitisha shughuli za uchimbaji wa kifusi katika shimo hilo kwa kuwa unahatarisha usalama na maisha ya wakaaazi wa eneo hilo lakini pia ni kinyume na utaratibu kwa kuwa eneo hilo halikuruhusiwa kisheria kwa shughuli hizo.
