RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema kuwa bila ya maendeleo endelevu yenye tija katika sekta ya kilimo amani na utulivu uliopo utatetereka kwa sababu ya kudhoofika kwa sekta hiyo na kuathiri hali ya uhakika wa chakula.
Dk. Shein aliyasema hayo katika ufunguzi wa Maonyesho ya Nane Nane yaliyofanyika huko Langoni, Wilaya ya Magharibi “A” Mkoa wa Mjini Magharibi ambayo yalihudhuriwa na viongozi mbali mbali wa vyama vya siasa na Serikali akiwemo Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd pamoja na wananchi wengine.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein, akihutubia wakati akifungua Maonesho yua Maadhimisho ya Siku ya Wakulima Nanenane Zanzibar,uliofanyiuka katika viwanja vya Kizimbani Wilaya ya Magharibi "B"Unguja leo 4/8/2020.
Rais Dk. Shein alisema kuwa uhakika wa chakula unapoathirika mifumko ya bei huzuka kwa kile chakula kidogo kilichopo hivyo, watakuwepo watakaomudu na watakaoshindwa kukabiliana na mifumko hiyo.
Hivyo, alisema kuwa malalamiko, bughudha, hasira na chuki zitakuwa haziishi kwani njaa inazaa athari nyingi mbali ya hizo za kisaikolojia lakini hata za kiafya sambamba na kuondoa subira na uvumilivu, mambo ambayo yanaweza kupelekea utendaji wa maovu mbali mbali na kusababisha kuvunjika kwa amani na utulivu.
Rais Dk. Shein alisema kuwa ukosefu wa amani na utulivu si kama tu unazuia jitihada za maendeleo zisifanikiwe bali unateketeza mpaka yale maendeleo ambayo yalikwishafikiwa kama ambavyo nzige wanavyoteketeza mazao shambani.
“Mwenyezi Mungu atuepushie mbali nchini mwetu na awaondoshee wenzetu waliofikwa na balaa hilo la kukosa amani na utulivu”,alisisitiza Rais Dk. Shein.
Alieleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuzingatia umuhimu wa uhakika wa chakula na lishe na uimarishaji wa kilimo endelevu, imekuwa ikitekeleza kwa vitendo Sheria Namba 5 ya mwaka 2011 ya Uhakika wa Chakula na Lishe Zanzibar.
Alisema kuwa katika mwaka wa fedha 2020/2021, Serikali imeongeza bajeti ya Kilimo kutoka TZS Bilioni 88.17 ya mwaka 2019/2020 hadi kufikia TZS Bilioni 129.86 kwa mwaka 2020/2021.
Alieleza kuwa mambo mengi katika sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi na kusisitiza kuwa miongoni mwa mambo ambayo Serikali imeyafanya ni kujenga miundombinu ya umwagiliaji maji katika hekta 1,524 Unguja na Pemba kutokana na mkopo wa dola za Kimarekani milioni 59 kutoka Benki ya Exim ya Jamhuri ya Korea.

