Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi Zanzibar ZAECA imesema kwamba tayari imetoa elimu kwa watendaji na wasimamizi wa fedha wa Mabaraza ya Manispaa na Halmashauri lengo ni kuondoa kasoro ambazo zimekuwa zikijitokeza katika utoaji wa zabuni, ukusanyaji wa mapato na matumizi ya fedha za Serikali.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mkuu wa ZAECA Ali Abdalla Ali alipofika Afisi ya Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi kwa ajili ya kujitambulisha pamoja na kuelezea juu ya hatua ambazo Mamlaka yake imekuwa ikiendelea kuzichukua.
Amesema ZAECA imebaini kuwa kumekuwa na dosari nyengine zimekuwa zikifanywa na watendaji na wasimamizi wa fedha pasipo kujua na hatimaye hujikuta wakiingia kwenye makosa, kwa hiyo wameona kuna haja ya kutoa elimu kwa wahusika ili kuondoa kasoro na dosari hizo walizozibaini.
Kwa upande mwengine ameeleza kuwa ZAECA wanaendelea kupitia miradi ya maendeleo inayotekelezwa nchini ili kuhakikisha fedha zinazokwenda kwenye miradi hiyo zinatoka na kutumika kwa kufuata utaratibu na sheria ziliyopo.
Aidha amesema mbali na miradi hiyo ZAECA wanaendelea kufanya ukaguzi wa miradi yote iliyozinduliwa wakati wa Mbio za Mwenye wa Uhuru kwa upande wa Zanzibar ili kuangalia kama fedha zilizotumika kwenye miradi hiyo zinawiana miradi yenyewe.
Mkurugenzi huyo amesema kwamba kwa sasa ZAECA wamejipanga kuhakikisha wanakwenda kudhibiti vitendo vya rushwa na uhujumu uchumi ili kuzuia matukio hayo kabla ya kutokea na kuleta athari kwa taifa na wananchi wake.
Naye Mkuu wa Mkoa Mjini Maharibi Idrisaa Kitwana Mustafa amemueleza Mkurugenzi huyo kuwa Mkoa utaipa mashirikiano ya karibu ZAECA ili iweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.
Amempongeza Mkurugenzi huyo kwa hatua zinazoendelea kuchukuliwa na Taasisi yake katika kukabiliana na vitendo vya rushwa na uhujumu uchumu tangu ateuliwe kushika nafasi hiyo.