Wizara ya Elimu na Mafuzo ya Amali imesisitiza haja ya kuwepo mashirikiano baina ya Wizara hiyo na Serikali ya Mkoa Mjini Magharibi ili kufanikisha awamu ya pili ya programu ya kuwarudisha Skuli watoto wapatao 5,960 walio nje ya mfumo rasmi wa elimu ya msingi ndani Mkoa huo.
Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Ali Abdulgulam Hussein ametoa ushauri huo katika kikao kilichowakutanisha uongozi wa Wizara hiyo na uongozi wa Mkoa Mjini Magharibi kupanga mikakati itakayofanikisha mpango wa kuwarudisha watoto hao Skuli.
Akizungumza katika kikao hicho kilichofanyika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi, Hussein amesema kwamba Wizara imeona kuna umuhimu mkubwa wa kushuka Mikoani ili kupanga mikakati ambayo itasaidia kufikia malengo ya kuwarejesha Skuli watoto wote waliolengwa katika utekelezaji wa programu hiyo.
Amesema Wizara imebaini changamoto mbali mbali katika utekelezaji wa programu hiyo awamu ya kwanza kwa hiyo bila ya kuwepo mashirikiano ya pamoja ya Wizara na Mikoa, awamu ya pili ya zoezi hilo itakuwa vigumu kuweza kufanikiwa.
Naibu Waziri amesema lengo la Wizara ya Elimu ni kuona watoto wote wenye umri kati ya miaka 7 hadi 14 waliyoacha Skuli kwa sababu mbali mbali wanarejeshwa Skuli ili kuendelea kupata elimu hasa ikizingatiwa kuwa suala la elimu ni haki yao ya msingi kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984.
Amebainisha kuwa idadi ya wanafunzi waliyo nje ya mfumo wa elimu ya msingi kwa Zanzibar bado ni kubwa na kutaka kuwepo kwa mashirikiano ya wadau wote wa elimu ili kujenga hamasa na ushawishi kwa wazazi kuhakikisha kuwa watoto wao wanarudi Skuli kupata elimu.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Idrissa Kitwana Mustafa ameihakikishia Wizara hiyo kuwa Mkoa utayafanyia kazi maamuzi yote waliyokubaliana nayo katika kutekeleza mpango huo.
Hata hivyo amesema kuwa wakati umefika wa kuwepo sheria ndogo ndogo zitakazochukuliwa dhidi ya wazazi na walezi watakaobainika kushindwa kuwasimamia watoto wao kuweza kupata elimu yao ya msingi.
Aidha ameishauri Wizara kujenga Skuli za maandalizi, msingi na sekondari ndani ya Mkoa Mjini Magharibi katika maeneo ambayo watoto wamekuwa wakitembea masafa marefu kwenda Skuli.
Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa programu hiyo Mkurugenzi Idara ya Elimu Mbadala na Watu Wazima Mashavu Ahmada Fakih ametaja baadhi ya changamoto zilizopelekea utekelezaji wa zoezi hilo awamu ya kwanza kushindwa kufikia malengo kuwa ni pamoja na muitikio mdogo wa wanajamii kuwarejesha watoto Skuli na mashirikiano duni miongoni mwa wadau.
Amesema kwamba Mkoa Mjini Magharibi unajumla ya watoto 8,301 waliotakiwa kurejeshwa Skuli ambapo jumla ya watoto 2,341 waliweza kurejeshwa Skuli katika awamu ya kwanza ya zoezi hilo lililofanyika Julai 2021 hadi Mei 2022.
Mkurugenzi huyo amesema programu hiyo inaenda sambamba na ujenzi na ukatabati wa madarasa na vyoo, mafunzo ya walimu, ununuzi wa vifaa vya kujifunzia na kufundishia na zoezi la uhamasishaji wa jamii.
Programu hiyo ya miaka mitatu inatekelezwa katika Wilaya zote kumi na moja za Zanzibar na kusimamiwa na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kwa Kushirikiana na Shirika la UNICEF na Taasisi ya Education Above All ya Nchini Qatar ambapo hadi kukamikimilika kwake mwaka 2024 inatarajiwa kutumia jumla ya dola za kimarekani 6,002,620.