OFISI YA RAIS
TAWALA ZA MIKOA NA IDARA MAALUM ZA SMZ

OFISI YA MKUU WA MKOA MJINI MAGHARIBI

Home>>Habari>>Wajasiriamali wahimizwa kurejesha mikopo
HabariHabari Mpya

Wajasiriamali wahimizwa kurejesha mikopo

Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Mhe. Idrissa Kitwana  Mustafa amevihimiza vikundi vya wajasiriamali  kurejesha kwa wakati uliopangwa mkopo  wa boti za uvuvi ili  kuweza kuvikopesha vikundi  vyengine .

Amesema hayo  huko Afisini kwake Vuga wakati wa kikao cha kufanya tathmini kuhusu  vikundi vilivyopewa mikopo ya boti kilichoshirikisha Wakuu wa Wilaya, watendaji wa Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi, Wizara ya Kazi na Uwezeshaji, taasisi ya Rais ya tathmimi na ufuatiliaji na benki ya CRDB.

 Amesema bado kuna vikundi vingi vya wajasiriamali vinasubiri kupatiwa mikopo, hivyo ili Serikali iweze kuendelea kutekeleza mpango huo ni vyema wakahakikisha wanarudisha mikopo hiyo.

Ameitaka Benki ya CRDB inayosimamia utoaji wa mikopo kwa wajasiriamali kuweka mazingira mazuri yatakayoviwezesha vikundi vilivyokopa kurudisha mikopo kwa wakati uliyopangwa.

Aidha Mkuu wa Mkoa amesema inaonekana elimu iliyotolewa kwa wajasiriamali bado haikutosheleza, hivyo ameziomba Wizara husika kuendelea kuvielimisha vikundi hivyo ili waweze kunufaika na mikopo waliyopatiwa.

Amefahamisha kuwa Serikali ya Mkoa ina dhamira ya dhati kuona mipango ya Serikali na ilani ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2020-2025 kwa upande wa kuwawezesha wananchi inatekelezwa kikamilifu.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi Abuod Suleiman Jumbe amesema kuwa zaidi ya milioni mia tatu tayari zimeshatolewa kwa vikundi vya wavuvi  vya Mkoa Mjini Magharibi ikiwa ni katika  kutekeleza sera ya Serikali  ya awamu ya nane ya kuwawezesha wananchi  kujikwamua kiuchumi.

Ameongeza kuwa Wizara yake imeweka mikakati mbali mbali kuhakikisha inazipatia ufumbuzi changamoto zinazojitokeza katika mpango huo .

Nae meneja CRDB Tawi la Zanzibar Makame Hassan amewasisitiza wajasiriamali hao kurejesha mikopo katika kipindi stahiki na endapo watakapokabiliwa na changamoto yoyote  watoe  taarifa mapema  kwa benki hiyo.

Nao wanavikundi wameomba kutatuliwa changamoto zinazowakabili ikiwemo kupewa elimu  ya namna ya kutumia vitendea kazi  vya kisasa  pamoja na kupatiwa boti kubwa zitakazowawezesha kuvua katika kina kikubwa cha bahari.