Wafanyakazi wa wizara, mashirika na taasisi mbali mbali wametakiwa kuwa waadilifu katika kusimamia mali za Serikali.
Ushauri huo umetolewa na Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Idrissa Kitwana Mustafa wakati akifunga Semina ya siku tano kwa wahasibu, washika fedha, wahakiki mali na maafisa manunuzi kuhusu usimamizi wa mali za Serikali iliyofanyika katika jengo la ZURA, Maisara.
Amesema kwamba upo mtindo kwa baadhi ya wafanyakazi wa kada hizo kufanya udanganyifu katika manunuzi na mauzo ya mali za umma kwa kutaka kujinufaisha wao binafsi na matokeo yake huitia hasara Serikali.
Amewataka mafunzo waliyoyapata katika semina hiyo kwenda kuyatumia katika kutekeleza majukumu yao sambamba na kufuata sheria na taratibu zinazowasimamia.
Mkuu wa Mkoa amesema kuwa mali za Serikai ni mali za umma, hivyo wafanyakazi hao wanadhima kubwa ya kudhibiti mali hizo hatua ambayo itaisaidia Serikali kutumia fedha zake katika mambo mengine ya maendeleo.
Kwa upande mwengine Mkuu wa Mkoa amempongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Husseina Ali Mwiniyi kwa kuunda Ofisi ya Msajili wa Hazina na Usimamizi wa Mali za Serikali ambayo amesema itasaidia sana kuhakikisha usalama wa mali za Serikali.
Akimkaribisha Mkuu wa Mkoa kufunga Semina hiyo Msajili wa Hazina kutoka Wizara ya Fedha na Mipango Wahid Mohammed Ibrahim Sanya amesema kumekuwepo na changamoto ya uharibifu wa mali za Serikali katika taasisi mbali mbali na kusema kuwa mafunzo hayo yatawawezesha wataalamu hao kusimamia kwa weledi mali za Serikali.
Nao wafanyakazi walioshiriki semina hiyo wameahidi kuongeza juhudi katika kuhakikisha mali za umma zinasimamiwa ipasavyo.