Afisa Ustawi wa jamii Mkoa wa Mjini Magharibi Bi Ramla Machano Haji amewataka Wazazi, Walimu na Walezi kuhakikisha kuwa wanasimamia vyema mienendo ya watoto hatua kwa hatua ili kuwaepusha na matendo ya udhalilishaji .
Bi Ramla amesema hayo wakati alipokuwa akitoa mafunzo juu ya athari za udhalilishaji kwa watoto huko katika skuli ya msingi Kiembe samaki A na B Mkoa wa Mjini Magharibi.
Amesema kuwa ni haki na wajibu kwa wazazi na walezi hao kuhakikisha kuwa watoto wanakuwa salama muda wote wanapokuwa majumbani na hata wanapokuwa skuli. Amesema udhalilishaji kwa watoto unaleta athari za kimwili, kiakili na kisaikolojia hali inayompelekea mtoto kushuka kwa kiwango cha ufahamu anapokuwa skuli.
Aidha Bi Ramla ameitaka jamii kuacha matendo ya udhalilishaji kwa watoto ili kumlinda mtoto kimaadili na kumjengea maisha bora ya sasa na ya baadae.
Nae Afisa Watu wenye Ulemavu Mkoa wa Mjini Magharibi Bi Salama Said ameitaka jamii kuacha tabia ya kuwadhalilisha watu wenye ulemavu kwa kuwaita majina yasiofaa kwani kufanya hivyo kunaleta athari kwa watu hao.
Kadhalika amekemea tabia inayofanywa na baadhi ya wazazi na walezi kuwafungia ndani Watoto wenye ulemavu kwa visingizio mbali mbali kwani kufanya hivyo kunapelekea kukosa haki za msingi kwa watoto hao ikiwemo kupata elimu.
Wakizungumza kwa niamba ya wanafunzi wenzao wa skuli hizo Yahya Hamadi Ali na Khadija Said Kombo wamewaasa wanafunzi wenzao kutoshawishika na jambo lolote lenye madhara kwao na kuto kujilinda na vitendo vya udhalilishaji badala yake kutumia muda wao wote kwenye masomo na kazi za majumbani.