OFISI YA RAIS
TAWALA ZA MIKOA NA IDARA MAALUM ZA SMZ

OFISI YA MKUU WA MKOA MJINI MAGHARIBI

Home>>Habari>>TRA yapongweza kwa kufikia malengo ya makusanyo 2022-2023
HabariHabari Mpya

TRA yapongweza kwa kufikia malengo ya makusanyo 2022-2023

Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Idrissa Kitwana Mustafa ameipongeza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kwa kufikia malengo ya makusanyo ya kodi kwa mwaka uliopita. Amesema mafanikio hayo yanaonesha ni kwa namna gani wanavyojituma na kufanya kazi kwa weledi katika kufikia malengo waliyojiwekea.

Idrissa ametoa pongezi hizo katika kilele cha maadhimisho ya wiki ya shukurani kwa walipa kodi kwa mwaka fedha 2022-2023 iliyofanyika Hoteli ya Golden Tulip, Kiembesamaki.

Amesema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inafarajika na utendaji wa Mamlaka hiyo na itaendelea kushirikiana na taasisi zote zinazokusanya kodi Ili kuhakikisha malengo ya Serikali ya kuongeza mapato yake inafikiwa.

Mkuu huyo wa Mkoa vilevile amewahimiza watumishi wa TRA na Mamlaka nyengine zinazosimamia makusanyo ya kodi kuhakikisha wanaendelea kuwajibika pamoja na kufuata maadili ya kazi yao ili kujenga imani Kwa walipa kodi.

Aidha amewataka  wananchi kuendelea kulipa kodi kwa vile mapato ya fedha  zitokanazo na kodi   ndizo zinazoiwezesha Serikali ya awamu ya  nane inayoongozwa na Dkt.Hussein Ali Mwinyi  kutekeleza miradi ya maendeleo katika sekta mbali mbali nchini.

Wakati huo huo Mkuu wa Mkoa ameisifu TRA kwa kutambua umuhimu wa walipa kodi na  kuwazawadia walipa kodi  bora na kusema kuwa utamaduni huo umekuwa ukiihamasisha jamii kulipa kodi bila shuruti

Amewashauri waliyopata tuzo za walipa kodi bora kwa mwaka 2022-2023 kuendeleza mashirikiano na Mamlaka za kodi na wawe wazalendo ili malengo yanayowekwa na Serikali yaweze kufikiwa.

Akizungumza kwa niaba ya Kamishna Mkuu wa TRA, Mkurugenzi wa Fedha TRA kutoka Makao Makuu Dina Edward amefahamisha kwamba mapato ya TRA yamekuwa yakiimarika mwaka hadi mwaka kutokana na mipango na mikakati waliyojiwekea ikiwemo uimarishaji wa mifumo, uboreshaji wa mfumo wa ukusanyaji wa mapato ya ndani na kurahisisha taratibu za kulipa kodi. Pia amesema katika kupambana na rushwa, Mamlaka imekuwa ikishirikiana na taasisi husika kuwachukulia hatua za kisheria watumishi wanaojihusisha na vitendo hivyo.

Naye Naibu Kamishna wa TRA Zanzibar, Saleh Haji Pandu amesema kwa mwaka wa fedha 2022-2023 walilenga kukusanya Shilingi Bilioni 400, hata hivyo wameweza kuvuka lengo  na kukusanya Bilioni 455. Ameeleza kwamba fedha zote zinazokusanywa na TRA hapa Zanzibar zinakwenda mfuko wa hazina wa SMZ na zinatumika kwa shughuli za maendeleo ya Zanzibar.

Mkurugenzi wa PBZ Dk. Muhsin Salim Masoud amewashukuru wateja wa Benki hiyo kwa mchango wao uliyowapelekea kushinda nafasi ya kwanza katika makundi tofauti ya walipa kodi. Amesema PBZ inatambua umuhimu wa kodi katika maendeleo ya nchi hivyo itaendelea kulipa kodi zote zinazotakiwa na Serikali.

Benki wa Watu wa Zanzibar (PBZ) imeshika nafasi ya kwanza ya mlipa kodi bora wa kodi za ndani, nafasi ya kwanza mlipa kodi mwenye mchango mkubwa na mshindi wa jumla kwa mwaka 2022-2023.