OFISI YA RAIS
TAWALA ZA MIKOA NA IDARA MAALUM ZA SMZ

OFISI YA MKUU WA MKOA MJINI MAGHARIBI

Home>>Habari>>Tengeni fedha kuhifadhi mazingira: Kiongozi wa Mwenge wa Uhuru
HabariHabari Mpya

Tengeni fedha kuhifadhi mazingira: Kiongozi wa Mwenge wa Uhuru

Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Abdallah Shaib Kaim amezitaka Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kutenga bajeti ndogo ndogo ambazo zitakwenda kuongeza nguvu katika kutunza mazingira pamoja  na kampeni za upandaji wa miti.

Ametoa rai hiyo  alipokuwa  akihutubia viongozi na wananchi wa Wilaya ya Mjini kuhusu ujumbe wa Mwenge wa Uhuru mwaka 2023  katika viwanja vya Maisara.

Amesema moja ya malengo ya  mbio za Mwenge wa Uhuru  mwaka huu ni kuwakumbusha viongozi wa Serikali za Mitaa  juu ya umuhimu wa uhifadhi wa mazingira ili kuliepusha taifa dhidi ya majanga mbali mbali ikiwemo  ukame, kuongezeka kwa joto na mafuriko.

Aidha amewataka wananchi kuacha tabia ya uharibifu wa mazingira kwa kukata miti ovyo, kuchoma misitu na kufanya shughuli za ufugaji na kilimo karibu na vianzio vya maji.

Akizungumzia vita dhidi ya rushwa Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru amesema kuwa rushwa bado ipo na imekuwa ikiathiri utoaji wa huduma za umma na ujenzi wa miradi ya serikali.

Amewahimiza wananchi   kushirikiana na taasisi ya kupambana na rushwa ZAECA kwa kutoa taarifa zinazohusiana na vitendo hivyo.

Amesema wakati umefika  kutokomeza rushwa kivitendo kwa kukataa kutoa na kupokea  pamoja na  kuwa tayari kusimama  mahakamani kutoa ushahidi juu ya masuala yanayohusu rushwa.

Kuhusu ujumbe wa mapambano dhidi ya UKIMWI Abdallah amewataka wananchi kujenga tabia ya kupima kwa  hiari ili kuweza kujitambua na kuacha tabia hatarishi zinazopelekea kupata maambukizi ya virusi hivyo.

Akielezea juu ya ujumbe wa vita dhidi ya maleria amesema bado maradhi hayo yapo na ndio yanayoongoza kwa vifo nchini hivyo amewahimiza  wananchi wa Wilaya ya Mjini kutumia vyandarua ,kufika vituo vya afya kupima afya zao, kutumia dawa za maleria kwa usahihi na kuondoa madimbwi na vichaka karibu na makaazi yao.

Kiongozi wa mbio za Mwenge amewaasa pia vijana kutumia fursa mbali mbali ziliyopo katika kujipatia kipato badala ya kujiingiza kwenye biashara ya madawa ya kulevya.

Vilevile aliwataka wazazi kufuatilia kwa karibu nyendo za vijana wao ili kuwanusuru kujiingiza kwenye matumizi ya madawa hayo.

Mwenge wa Uhuru ulikimbizwa takribani kilomita 13 ndani ya Wilaya ya Mjini ambapo Kiongozi na wakimbiza Mwenge wa Uhuru Kitaifa, viongozi na wafanyakazi  wa Mkoa, Wilaya, Manispaa  pamoja na wananchi walishiriki katika zoezi la upandaji wa miti, kupima afya,    kuzuru kaburi la Marehemu Mzee Abeid Amani Karume, kukagua mazingira Soko la Darajani na kukagua vijana wanaojishughulisha na kazi za sanaa Vuga.