Mwenyekiti wa Tume ya Kuboresha Taasisi za Haki Jinai, Jaji Mkuu Mstaafu wa Tanzania Mohamed Chande Othman amesema nia ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kuunda Tume hiyo ni kuimarisha mfumo wa utendaji wa taasisi hizo ili wananchi waweze kuwa na imani nazo pamoja na kutoa mashirikianao yao.
Ameyasema hayo kwenye ukumbi wa Sheikh Idrissa Abdull Wakili Kikwajuni, Wilaya ya Mjini katika mkutano uliyohudhuriwa na viongozi wa dini wa madhehebu mbali mbali pamoja na makundi maalum.
Amezitaja taasisi zinazohusika na masuala ya haki jinai kuwa ni pamoja na Jeshi la Polisi, Ofisi ya Mwendesha Mashtaka, Mahkama na magereza ama Vyuo vya Mafunzo kwa Zanzibar.
Amewataka wananchi watakaopata nafasi ya kushiriki kwenye mikutano kama hiyo kuwa huru kuelezea changamoto ziliyomo katika taasisi za haki jinai pamoja na kutoa maoni na mapendekezo yao yatakayosaidia kuimarisha utendaji kazi wa taasisi hizo.
Jaji Othman amesema tayari tume yake imeshakutana na wananchi wa makundi mbali mbali katika Mikoa 18, Wilaya 50 na kutembelea magereza 19 huku zoezi hilo likiendelea katika Mikoa mengine ya Tanzania Bara na Zanzibar.
Ameeleza kuwa matokeo ya Tume hiyo yatategemea sana hali halisi kupitia maoni wanayokusanya kutoka kwa wananchi na mazingira watakayoyaona kwenye taasisi za haki jinai.
Baadhi ya Viongozi wa dini na wananchi waliozungumza katika mkutano huo wametaja changamoto kadhaa zilizomo katika taasisi za haki jinai ikiwemo rushwa, kucheleweshwa kwa uchunguzi wa kesi, watuhumiwa kukaa muda mrefu rumande bila kuhukumiwa, miundombinu isiyo rafiki kwa wenye mahitaji maalumu kwenye vituo vya polisi na majengo ya magereza yasiyozingatia haki za binaadamu.
Aidha wametoa ushauri, maoni na mapendekezo yao mbali mbali sambamba na kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuunda chombo hicho kwa ajili ya kuboresha mfumo wa utendaji kazi wa taasisi za haki jinai nchini.
Tume ya Kuboresha Taasisi za Haki Jinai ilianza kutekeleza majukumu yake tarehe 1 febuari, 2023 na inatarajiwa kukamilisha ndani ya miezi minne.