Makamu wa Kwanza wa Rais Mhe. Othman Masoud Othman amefungua mradi wa maji safi na salama Skimu ya Masingini, Wilaya ya Magharibi ‘A’.
Akihutubia wananchi waliohudhuria hafla hiyo ikiwa ni katika muendelezo wa matukio ya Maadhimisho ya Sherehe za Kutimiza Miaka 60 ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mhe. Othman amesema Serikali ya Awamu ya Nane itaendelea na jitihada zake za ujenzi wa miradi ya maji safi na salama hadi pale itakapohakikisha wananchi wote wa Zanzibar wanapata huduma hiyo kama ambavyo ilidhamiriwa na waasisi wa Mapinduzi ya Zanzibar ya Mwaka 1964.
Aidha ameutaka Mkoa, Wilaya na Mabaraza ya Manispaa kuendelea kutoa ushirikiano wao kwa Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA) hata baada ya mradi huo kukamilika na kuanzia kuwahudumia wananchi.
Mbali na hayo amewataka wananchi kuitunza miundombinu ya maji na kulipia huduma hiyo ili iweze kuwa endelevu.
Akitoa salamu za Wananchi wa Mkoa Mjini Magharibi, Mkuu wa Mkoa huo ldrissa Kitwana Mustafa ameipongeza ZAWA kwa juhudi kubwa waliyoichukua na kuweza kukamilisha mradi huo unaokwenda kuwanufaisha wananchi 140,000 katika Shehia ya Masingini, Mwera, Kianga na Mtofaani.
Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji Zanzibar Mhandisi. Dkt. Salha Mohammed Kassim amesema kazi iliyofanyika katika Skimu ya Masingini ni pamoja na ujenzi wa tangi la chini lenye uwezo wa kuhifadhi maji lita milioni 14, tangi la juu lita milioni 4 na usambazaji wa mabomba yenye urefu wa kilomita 44.