OFISI YA RAIS
TAWALA ZA MIKOA NA IDARA MAALUM ZA SMZ

OFISI YA MKUU WA MKOA MJINI MAGHARIBI

Home>>Habari>>RC Kitwana afanya mazungumzo na Bishop Shayo
HabariHabari Mpya

RC Kitwana afanya mazungumzo na Bishop Shayo

Mkuu wa  Mkoa Mjini Magharibi Mhe. Idrissa Kitwana Mustafa amesema Serikali  itahakikisha wananchi wa Mkoa huo wanaendea kuishi pamoja  licha ya tofauti zao za imani ya  dini tofauti.

Amesema hayo  alipokuwa na mazungumzo na Askofu wa Kanisa Katoliki Zanzibar, Bishop Augustine Shayo  wakati alipofika katika Kanisa hilo hapo Forodhani, Wilaya ya Mjini kufuatia tukio lililotokea mwishoni mwa wiki iliyopita la kijana mmoja kuingia ndani ya Kanisa na kuvunja baadhi ya masanamu.

Akiwa pamoja na Kamati yake ya Usalama ya Mkoa katika mazungumzo hayo, Mkuu wa Mkoa amemueleza Bishop Shayo kuwa Serikali ya Mkoa imeguswa na tukio hilo na tayari imeshavielekeza vyombo vyote husika kuchukuwa hatua kwa mujibu wa sheria na taratibu ziliopo.

Aidha Mkuu wa Mkoa amempa pole Kiongozi huyo kwa tukio hilo na kusema kuwa Serikali imelichukulia tukio hilo kwa uzito ule ule uliochukuliwa na Kanisa Katoliki.

Kwa upande mwengine Idrissa amewahimiza wananchi wa Mkoa Mjini Magharibi kuendelea kuheshimu dini ya kila mmoja ili jamii iweze kuendelea kuishi kwa amani na utulivu.

Naye Askofu wa Kanisa Katokili Zanzibar, Bishop Augustine Shayo amesema kuwa Kanisa imelikabidhi suala hilo kwa vyombo husika na lina imani kuwa italifanyia kazi kwa mujibu wa sheria.

Ameeleza pia kufarajika kwake na uamuzi wa viongozi wa Mkoa kufika katika kanisa hilo kwa ajili ya kutoa pole pamoja na kuelezea hatua walizoanza kuzichukuwa.

Akizungumza kwa niaba ya Kamanda wa Polisi Mkoa Mjini Magharibi ACP Cleophace Magesa amesema Jeshi la Polisi linafanya uchunguzi wa kina ili kubaini kama kuna watu wengine wanaohusika na tukio hilo.