Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Idrissa Kiwana Mustafa ameziagiza Wilaya kuratibu na kufanya tathmini ya haraka ya miundo mbinu na makaazi ya watu waliyoathirika na mvua kubwa zilizonyesha mwishoni mwa wiki iliyopita.
Agizo hilo amelitoa wakati wa ziara yake yenye lengo kuwafariji wananchi pamoja na kukagua maeneo yaliyoathirika na mvua hizo katika ya Wilaya ya Mjini, Magharibi A na B.
Akizungumza mara baada ya kukagua maeneo hayo, Mkuu wa Mkoa amawataka Wakuu wa Wilaya kushirikiana na Masheha kuhakikisha kazi ya kuwatambua wananchi waliyoathirika pamoja na tathmini yake inafanyika kwa usahihi ili Serikali iangalie namna itakavyoweza kuwasaidia wananchi hao.
Kwa upande mwengine Idrissa amewasisitiza wananchi ambao nyumba zao zimeingia maji kutorudi katika nyumba hizo hadi Serikali itakapozipiga dawa ili kuepukana na maradhi ambayo yanaweza kutokea kutokana na maji ya mvua kuchanganyika na maji ya vyoo na karo katika maeneo hayo.
Amesema Serikali ya Mkoa kwa kushirikiana na Wizara husika imeanza kuchukua hatua ili kuona nyumba hizo zinapigwa dawa kabla ya wakaazi wake kurudi kwenye makaazi yao.
Sambamba na hayo Mkuu wa Mkoa amewataka wakaazi wa Mkoa huo hasa wa maeneo ya mabondeni kuchukua tahathari na kuhama katika maeneo hayo kwa vile bado mvua kubwa zinatarajiwa kuendelea kunyesha katika kipindi hiki.
Wakati huo huo Idrissa alifika Sebleni kutoa mkono wa pole kwa familia ya kwa marehemu Abubakar Abdalla Othman aliyefariki siku ya Jumaapili baada ya kuzama katika mtaro wa maji ya mvua wakati akijaribu kutoa taka zilizoziba kwenye mtaro huo. Ameiomba familia ya marehemu kuwa na subra katika kipindi hiki kigumu na kusema kuwa Serikali ipo pamoja nao katika msiba huo.
Zaidi ya nyumba 1,400 ziliingia maji katika Mkoa Mkoa Mjini Magharibi kufuatia mvua kubwa iliyonyesha siku ya jumapili huku baadhi ya kaya zikiwa bado zimehifadhiwa na majirani na nyengine zikilazimika kuhama katika maeneo hayo.