Serikali ya Mkoa Mjini Magharibi umezitaka Wizara mbali mbali kuushirikisha kikamilifu Mkoa huo katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Kauli hiyo imetolewa na uongozi wa Mkoa huo katika kikao chake na watendaji wa Wizara ya Maji Nishati na Madini na Wizara ya Ujenzi Mawasiliano na Uchukuzi kilichofanyika kwenye ukumbi wa mikutano ZURA kwa lengo lengo la kutatua changamoto za miundo mbinu ya maji na umeme zilizojitokeza katika ujenzi wa barabara unaoendelea maeneo mbali mbali ya Mkoa Mjini Magharibi.
Akizungumza katika kikao hicho, Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Mhe. Idrissa Kitwana Mustafa amesema kama Mkoa ndio wenye wajibu kisheria wa kuratibu na kusimamia miradi yote ya maendeleo kwenye Mkoa wake, sekta husika zinapaswa kuushirikisha vilivyo Mkoa katika utekelezaji wa miradi hiyo.
Amesisitiza kuwa iwapo sekta hizo zitakaa pamoja na Mkoa tangu hatua za awali za utekelezaji wa miradi, itaweza kusaidia kupunguza changamoto na malalamiko ya wananchi yanayojitokeza wakati miundo mbinu hiyo ikijengwa.
Aidha Mkoa imezitaka Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA) na Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO), kuchukua juhudi za haraka kurudisha huduma kwa wananchi katika maeneo ambayo yameathirika na ujenzi wa barabara.
Naye Katibu Mkuu Wizara ya Maji Nishati na Madini Joseph Kilangi amesema kuna haja ya kuimarisha mashirikiano baina ya Wizara zote husika pamoja na Mkoa ili changamoto kama hizo zisijitokeze tena kwenye maeneo mengine ya ujenzi wa barabara.
Nayo Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA) na Shirika la Umeme (ZECO) wameshauri katika ujenzi wa barabara mbali mbali za Mkoa Mjini Magharibi kuachwa eneo la kutosha la hifadhi ya barabara kwa ajili ya kupitisha miundo mbinu yao ya maji na umeme. Jumla ya Kilomita 90.9 za barabara za lami zitajengwa ndani ya Mkoa Mjini Magharibi katika mradi huo