Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Idrissa Kitwana Mustafa amewataka watendaji wa Mkoa, Wilaya na Manispaa za Mkoa huo kuwahamasisha wananchi na sekta mbali mbali kuchangia Mbio za Mwenge wa Uhuru za Mwaka 2022.
Agizo hilo amelitoa hapo Afisi ya Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Vuga wakati akizindua Kamati mbali mbali zitakazosimamia Mbio za Mwenge wa Uhuru katika Mkoa huo.
Amesema pamoja na kuwa mchango huo ni wa hiari, ni vyema kuwaelimisha wananchi juu ya umuhimu wa michango yao kwa vile imekuwa ikitumika kuendeleza miradi mbali mbali ya maendeleo hasa iliyoanzishwa na wananchi wenyewe.
Amesema Mwenge wa Uhuri hauna itikadi ya Chama au kundi lolote lile, hivyo amaewataka watendaji hao kuwashirikisha wananchi na taasisi zote ziliomo ndani ya Mkoa huo kuchangia Mbio za Mwenge wa Uhuru za Mwaka huu.
Mkuu wa Mkoa amesema Serikali ya Mkoa inadhamini mchango wowote ule utakaotolewa na mwananchi au taasisi yoyote ile kwani utasaidia kuimarisha huduma za kijamii kwenye Mkoa wake.
Adha amezitaka Kamati hizo kutekeleza majukumu yao ipasavyo ili kufanikisha suala zima la ukusanyaji michango pamoja na Mbio za Mwenge wa Uhuru katika Mkoa Mjini Magharibi na kuweza kuuletea ushindi Kiwilaya.
Mwenge wa Uhuru unatarajiwa kukimbizwa ndani ya Mkoa Mjini Magharibi kuanzia tarehe 23 hadi 25 Mei, 2022 ukitokea Mkoa wa Kusini Unguja.