Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Mhe. Idrissa Kitwana Mustafa amesema Miaka 59 ya Muungano wa Tangayika na Zanzibar imeleta mafanikio na manufaa makubwa katika Mkoa wake.
Ameyasema hayo katika Sherehe za Kilele cha Maadhimisho ya Miaka 59 ya Muungano wa Tanzania zilizoadhimishwa Kimkoa katika viwanja vya Maisara, Wilaya ya Mjini.
Amesema moja ya mafanikio hayo ni uwepo wa hali ya amani na utulivu ambapo wananchi wa Mkoa huo wamekuwa wakifanya shughuli zao za kimaisha bila hofu na wasiwasi wowote kwa miaka yote 59 ya Muungano.
Ameeleza pamoja na amani na utulivu, Muungano umewanufaisha wananchi wa Mkoa wake kwa fursa mbali mbali zikiwemo fursa za ajira, elimu, biashara na nyenginezo ambazo zimekuwa zikiwapatia kipato mtu mmoja mmoja na pato la Serikali kupitia kodi zinazokusanywa.
Mkuu wa Mkoa ameeleza pia uwepo wa Taasisi za Muungano katika Mkoa huo zimesaidia sana kuimarisha utoaji wa huduma kwa wananchi na kuzitaja baadhi ya huduma hizo zikiwemo za kibenki, mawasiliano na afya.
Aidha Idrissa ameeleza kuwa kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii TASAF Mkoa wa Mjini Magharibi umenufaika na miradi mbali mbali ya maendeleo ngazi ya jamii pamoja na kuzisaidia kaya masikini kuweza kuinua kipato chao katika Shehia 121 za Mkoa huo.
Katika Sherehe hiyo, Mkuu wa Mkoa amewahimiza vijana kuendelea kuuenzi, kuulinda na kuutunza Muungano na kuachana na watu wanaoubeza Muungano kwa maslahi yao binafsi.
Akizungumza na hadhara iliyohudhuria maadhimisho hayo Professor Patrick Lumumba amesema Watanzania wanapaswa kujivunia Muungano wao na kuhakikisha unaendelea kudumu kwa msalahi ya vizazi vya sasa na vijavyo.
Naye Mkuu wa Wilaya Magharibi ‘A’ Suzan Peter Kunambi ameeleza kwamba Muungano wa Tanyanyika na Zanzibar umeweza kuondoa ubaguzi, ukabila, urangi na udini na kuwaunganisha Watanzania kuwa wamoja.
Sherehe za Muungano hufanyika kila ifikapo April 26 ambapo kwa mwaka huu zimefanyika kimkoa katika Mikoa yote ya Tanzania.