Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Mhe. Idrissa Kitwana Mustafa ametoa onyo kali kwa watu wanaotumia majina ya viongozi kuwatapeli wananchi wanohitaji huduma zinazotolewa na Serikali.
Amesema Serikali ya Mkoa Mjini Magharibi haitasita kuchukua hatua za kisheria dhidi ya watu wanaofanya vitendo hivyo ambavyo vinaoneokana kuongezeka siku hadi siku.
Mkuu wa Mkoa ametoa onyo hilo kufuatia kupokea malalamiko ya mwananchi mmoja ndugu Seif Mohammed Ali kudai kutapeliwa kiasi cha shilingi milioni kumi na moja na ndugu Khamis Suleiman Khamis ili kumpatia mlango wa duka katika kituo cha biashara cha Darajani Souk.
Akizungumzia kadhia hiyo mbele ya mlalamikaji na mlalamikiwa hapo afisini kwake Vuga, Mkuu wa Mkoa amesema kitendo kilichofanywa na mtuhumiwa huyo kutumia majina ya viongozi kuwatapeli wananchi wanyonge ni kinyume cha sheria, hivyo atahakikisha hatua za kisheria zinachukuliwa ili kukomesha tabia hiyo.
Mkuu wa Mkoa amewataka wananchi wanaohitaji milango ya maduka Darajani na huduma nyengine zinazotolewa na Serikali kuwa waangalifu dhidi ya matapeli kwani wamekuwa wakitumia mbinu mbali mbali kuwatapeli wananchi.
Aidha Mhe. Idrissa amewataka wananchi wa Mkoa wake kushirikiana na vyombo vya ulinzi kwa kutoa taarifa za watu wanaofanya vitendo hivyo ili waweze kuchukuliwa hatua za kisheria.
Amewataka pia wananchi kufuata taratibu katika kupata huduma zinazotolewa na taasisi mbali mbali za Serikali na zisizo za Serikali badala ya kuwatumia watu ambao hawahusiki na masuala hayo.
Kwa upande wake Katibu Tawala Mkoa Mjini Magharibi Moh’d Ali Abdalla ameelezwa kusikitiswa na vitendo vinavyofanywa na baadhi ya watu kujifanya watumishi wa umma kujipatia fedha kutoka kwa wananchi kwa njia za udanganyifu.